KESI INAYOWAKABILI MBUNGE WAITARA, MWANDISHI WA HABARI KUTOLEWA HUKUMU JUNI 16
Na Mwandishi Wetu, Musoma
KESI ya madai inayowakabili Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara ambaye ni mdaiwa namba moja, Karoli Jacob mdaiwa namba mbili na Mara TV mdaiwa namba tatu , itatolewa hukumu Juni, 16, 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma.
Wadaiwa wanakabiliwa na kesi ya madai shauri namba 23, ya mwaka 2023 iliyofunguliwa na Eliakim Chacha Maswi, aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma ( PPRA) , ambaye kwa sasa ni Katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.
Eliakim Maswi alifungua kesi kutaka wadaiwa kumlipa Tsh. Bilioni 12 kama fidia ya madhara ya jumla pamoja na Tsh. Bilioni moja kama fidia ya adhabu kwa madai ya kumkashfu.
Akizungumza nje ya viunga vya mahakama kuu Kanda ya Musoma, Mei, 14, 2025, Wakili wa Karoli Jacob , Ernest Mhagama amesema shauri limesikilizwa na wametoa ushahidi mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania , Kanda ya Musoma.
" Shauri limesikilizwa na leo ( Jana) , sisi ndio tulikuwa tunatoa ushahidi , shahidi wetu alitakiwa kutoa ushahidi na tumemwongoza kadri ya uwezo wetu .
" Kilichopo kwa sasa tunasubiri hukumu ambayo kimsingi itatoka tarehe 16 mwezi wa sita mwaka 2025 hapa mahakama kuu Kanda ya Musoma" amesema Wakili Ernest.
Wakili mwingine wa Karoli, Hekima Mwasipu ameongeza kusema " Upande wetu tumeshatoa utetezi mashahidi wameeleza . Mahakama imeridhia na mwenendo kwahiyo tunasubiri tu tarehe ya hukumu " amesema Wakili Hekima.
Mwandishi wa habari Karoli Jacob amesema " Tulifunguliwa shauri la madai Na. 23 , mwaka 2023 baada ya mchakato mzima ulioanzia mwaka 2023 hadi sasa.
Kushoto ni Wakili Hekima Mwasipu, katikati ni Mwandishi wa Habari Karoli Jacob, na kulia ni Wakili Ernest Mhagama wakiwa katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma.
" Jana (juzi) tulikuwa tunasikiliza ushahidi upande wa mleta maombi ambaye ni Eliakim Maswi na leo ( Jana ) upande wetu tumetoa ushahidi mbele ya Jaji anayesikiliza kesi hii Jaji Komba " amesema Karol.
>>Rejea
Machi , 19, 2023, Mahakama kuu Kanda ya Musoma ilimfungia mlango Mbunge Waitara ya kujitetea yeye na wenzake katika kesi inayowakabili iliyofunguliwa na Eliakim Maswi ambapo kesi hiyo inasikilizwa na kuamriwa upande mmoja.
Mahakama iliwafungia milango ya kujitetea kutokana na kushindwa kuwasilisha mahakamani majibu ya madai ya Eliakim kwa kuwasilisha maelezo ya utetezi wa awali kwa njia ya maandishi kabla ya usikilizwaji wa kesi hiyo, ndani ya muda unaotakiwa kisheria wa siku 21.
Wadaiwa hao walitakiwa kuwasilisha majibu yao ya utetezi ndani ya siku 21 tangu walipopewa hatua za wito wa mahakama lakini mpaka Machi, 13, 2024, kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya usikilizwaji walikuwa hawajawasilisha.
Wakili wa Waitara ,Hekima Mwasipu alidai kuwa alipewa na Waitara jukumu la kumwakilisha Januari 23, 2024, siku 21 zilikuwa tayari zimepitia, hivyo aliomba kuongezewa muda wa siku tano kuwasilisha majibu .
Wakili wa Karoli, Paul Bomani alidai kuwa mteja wake alichelewa kupata msaada wa uwakilishi mpaka Februari, 2024 alipopewa kazi hiyo na Baraza la Habari Tanzania ( MCT) na mwenzake Ernest Mhagama akipewa kazi hiyo na mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Novemba, 17, 2024.
Jaji Marlin Komba alikubaliana na sababu za pingamizi la Wakili Kassim Gilla ambaye ni Wakili wa Eliakim Maswi , kuwa hata muda ambao walipaswa kuomba kuwasilisha majibu yao nje ya muda ulishapita na kwamba wadaiwa walishindwa kutekeleza amri ya mahakama kuwasilisha majibu ndani ya siku 21.
Ikumbukwe katika hati ya madai Eliakim anadai kuwa Agosti, 9, 2023 , Waitara aliandaa mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na zaidi ya watu 500 katika Kijiji cha Mtana , Kata ya Manga, wilayani Tarime na kutoa maneno ya kashfa dhidi yake.
Anadai katika mkutano huo alisema Eliakim Maswi anahusika na anawajibika kwa vitendo vya rushwa kwa matumizi mabaya ya nafasi yake kama mtumishi wa umma katika nafasi ya mtendaji mkuu wa PPRA.
Eliakim anadai kuwa Agosti, 10, 2023, Waitara kwa kushirikiana na Karoli na Mara TV waliandaa wakapakia na kuchapisha katika televisheni ya mtandaoni ,katika chaneli ya YOUTUBE iitwayo Mara TV, maneno ya kashfa dhidi yake.
Anadai kuwa Agosti, 13, 2023 chapisho la maneno hayo yaliyorushwa na televisheni hiyo ya mtandaoni lilikuwa limetazamwa na watu 280 wa aina tofautitofauti duniani.
Post a Comment