HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: NI MISIMAMO KINZANI

WALISHASEMA zamani, yaingia akilini,

Usomtaka usoni, na kusema ni wa nini,

Kwa mwingine mdomoni, huyo anamtamani,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Adui wa msituni, akuchomaye machoni,

Kwa mwingine ni madini, ambayo yana thamani,

Wamtusi ya nguoni, amsifu hadharani,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Kila mtu wa thamani, hapa kwetu duniani,

Baradhuli wa moyoni, kwa mwingine ni mwandani,

Amemjaa moyoni, amwamini kama dini,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Bado hapa duniani, wapo wanaotamani,

Hitler Mjerumani, aloua milioni,

Ngekuwa bado enzini, watulie akilini,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Twasikia Musolini, wa kule Utaliani,

Fashisti na haini, na mwingi wa ufitini,

Kwa wengine huyo dini, vile wanamtamani,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Vile haiwezekani, ladha moja mdomoni,

Ndivyo mapenzi moyoni, kufananisha ni duni,

Umchukie fulani, mwingine penzi enzini,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Mtu kwenda kaburini, wengine wa furahani,

Sababu zao za ndani, hawafai duniani,

Waingia shereheni, na kula vitu laini,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Wengine wa majonzini, wameingia gizani,

Mpendwa hawamuoni, ametoweka jamani,

Na hata matumaini yanapotea hewani,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Uvumilivu mwilini, kwa misimamo kinzani,

Ni muhimu duniani, tukiwapo hadharani,

Tuugulie moyoni, kwa yale yaso makini,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Ni misimamo kinzani, yatawala duniani,

Kukubali wa gizani, wengine wako nuruni,

Hebu vumilianeni, ndivyo hivyo duniani,

Adui yako mkubwa, ni rafiki wa mwingine.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments