HEADER AD

HEADER AD

KATIBU WA AMCOS MASWA AFUNGWA JELA MIAKA 20

Na Samwel Mwanga, Maswa

MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu kwenda jela miaka 20 Katibu wa Chama Cha Ushirika cha Msingi(Amcos)Kijiji cha Gula,Masanja Mboje (36) baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya rushwa na uhujumu uchumi.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne Mei 20,2025 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo,Aziz Hamis baada ya mshtakiwa kukiri makosa yake kulingana na hati ya mashtaka katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 196/2025.

Pia mshtakiwa huyo ameamriwa kurejesha fedha Tsh 3,318,000/-ambazo alizifanyia ubadhirifu ikizingatiwa kwamba kati ya kiasi cha Sh 3,518,000/- alikuwa tayari amerejesha kiasi cha Sh 200,000.

Katibu huyo kwa mujibu wa hati ya mashtaka alifikishwa mahakamani hapo Januari 3,2025 akishtakiwa kwa makosa wawili ufujaji na ubadhilifu wa fedha .

Makosa hayo ni kinyume na Kifungu cha 28(2)cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,Sura 329 Marejeo ya Mwaka 2019,kikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwari la kwanza pamoja na vifungu vya 57(1)na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa sura 200 Marejeo ya mwaka 2022.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)Wilaya ya Maswa,Bahati Madoshi ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa akiwa Katibu wa Amcos ya Gula na mtu pekee aliyekasimiwa mamlaka ya kununua pamba kutoka kwa wakulima, alitumia kwa matumizi yake binafsi kiasi cha fedha Tsh. 3,518,000/- ambazo alipaswa kumlipa Edward Mathias baada ya kupeleka pamba yake yenye uzito wa kilo 2,268.



Ameendelea kuieleza mahakama kuwa kwa kufanya hivyo alikiuka mwongozo namba 1 wa msimu wa mwaka 2024/2025 kuhusu mfumo wa usimamizi na uuzaji wa pamba uliotolewa kwa Sheria ya tasnia ya pamba namba 2 ya mwaka 2011 unaotolewa na Bodi ya Pamba Tanzania.

Baada ya mahakama kumtia hatia mshtakiwa,kabla ya hakimu kumsomea adhabu,hakimu alitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea ambapo aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ni mgonjwa na ana mke na watoto wanaomtegemea.

“Kwa hiyo mahakama inakutia hatia mshtakiwaMasanja Mboje kwa makosa uliyoshitakiwa nayo,sasa mahakama hii inakuadhibu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela,pia umeamriwa kulipa sh 3,318,000/-ambazo ulizifanyia ubadhirifu, ” amesema hakimu,Aziz  Khamis.

Baada ya hukumu hiyo kusomwa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa(TAKUKURU) wilaya ya Maswa,Lucas Kuingwa amesema kuwa wakati mwenendo wa kesi hiyo ukiendelea na hatua ya uchunguzi kuna baadhi ya watu walilalamika kupitia mitandao ya kijamii kuwa taasisi hiyo imechukua rushwa na kushindwa kuendelea nayo jambo ambalo si kweli.

“Masuala ya uchunguzi wa kesi kama hizi ni mchakato na wakati mwingine huchukua muda mrefu ili kutafuta ushahidi ambao hauna shaka hivyo niiombe jamii kuwa na subira kuliko kuandika vitu vya upotoshaji mitandaoni na wakati mwingine kutaka kujichukulia sheria mkononi,”amesema.


 

 

No comments