KAMPUNI YA WARACHA YACHIMBA VISIMA VYA MAJI KUWAONDOLEA ADHA WANANCHI NYAMICHERE, NYAMANCHE
>>Wanakitongoji wasema kabla ya mradi wa maji waliamka alfajiri kutafuta maji kwenye vijito na visima vya wazi wakichangia na mifugo
Na Dinna Maningo , Tarime
KAMPUNI ya WARACHA inayojishughulisha na ujenzi na usambazaji wa vifaa, yenye makao yake makuu Nyamongo, katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, imechimba visima viwili vya maji ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya ukosefu wa maji.
Mradi huo utawanusuru wananchi ambao walikuwa wanachota maji yasiyo safi na salama kwenye mito, vijito na visima vya wazi visivyo safi na salama huku wakichangia na mifugo jambo ambalo si jema kiafya .
Visima hivyo ambavyo ni vya msaada, kimoja kimechimbwa katika Kitongoji cha Nyamichere na kingine katika Kitongoji cha Nyamanche Kijiji cha Nyakunguru , kata ya Kibasuka wilaya ya Tarime ,mkoani Mara, vyote vikigharimu Tsh. Milioni 45 fedha zilizotolewa na Kampuni ya WARACHA.
Asemavyo Mkurugenzi WARACHA
Mkurugenzi wa kampuni ya WARACHA, David Ryoba Tindo , kampuni inayofanya kazi zake Nyamongo, na wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ameeleza malengo ya mradi huo wa visima.
Mkurugenzi wa kampuni ya WARACHA, David Ryoba Tindo, ambaye kampuni yake ndio iliyochimba visima viwili vya maji katika Kitongoji cha Nyamanche na Nyamichere.
" Kampuni ya WARACHA imetoa msaada kwa kujenga visima viwili katika Kitongoji cha Nyamichere na Nyamanche ambapo uongozi wa serikali ya Kijiji ulituomba msaada tuwachimbie visima.
" Ni msaada ambao tumeona tuutoe kusapoti jamii zinazotuzunguka kutopata shida ya maji na kutotumia maji yasiyo safi na salama sambamba na kufanikisha maendeleo katika jamii zinazozunguka kampuni yetu na zinazozunguka mgodi wa North Mara" amesema David.
Amewataka wananchi kuyatumia vizuri maji hayo na kutunza miundombinu ya maji , kuhakikisha wanafanya usafi maeneo yanayozunguka mradi huo wa maji.
" Naomba maji haya yatumike vizuri kwasababu lengo la kuchimba hivi visima ilikuwa ni kupata maji safi na salama tofauti na maji ambayo mlikuwa mnayatumia ya mtoni na bwawani ambayo si salama.
" Visima hivi vimekuwa na uhitaji mkubwa , watumiaji wataongezeka . Tunzeni miundombinu ya maji iliyopo , kwasababu bila kuitunza haiwezi kukaa katika muonekano wa kudumu .
" Hakikisheni usafi unafanyika maeneo yanayozunguka visima, usalama wa Sola , pampu zinazosukuma maji na kuyatumia maji vizuri" amesema David.
Mkurugenzi mtendaji kampuni ya WARACHA, David Ryoba Tindo (kushoto) akiwa na Mwenyekiti Kitongoji cha Nyamanche Magweiga Chacha wakati wa ujenzi wa mradi wa maji.
Mgodi wa North Mara wapongezwa
Pia ameushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kuendelea kuzithamini kampuni za wazawa wanaoishi maeneo yanayozunguka mgodi kwa kuwapa zabuni mbalimbali ambazo zimewawezesha kujiinua kiuchumi na kuchangia maendeleo katika jamii wanazozizunguka.
" Tunaushukuru sana na kuupongeza mgodi wa Barrick North Mara kuendelea kushirikiana na makampuni ya wazawa ikiwemo kampuni ya WARACHA kwenye kazi mbalimbali .
" North Mara wanapotushika mkono na sisi tunapata nguvu za kuweza kurudisha kwenye jamii. Kazi wanazotupatia tunazifanya mwisho wa siku na sisi tunarudisha nguvu kwenye jamii kwa kuchangia maendeleo mbalimbali kama tulivyoweza kuchimba visima" amesema David.
Wananchi waipongeza WARACHA
Wananchi wa Kitongoji cha Nyamichere na Nyamanche wameipongeza kampuni ya WARACHA kwa msaada ya visima na kwamba kwa sasa wanatumia maji safi na salama yasiyo ya kuchangia na mifugo.
Mwenyekiti mstaafu Kijiji cha Nyakunguru Charles Marara, mkazi wa Kitongoji cha Nyamichere kwa zaidi ya miaka 50 amesema kabla ya mradi huo kulikuwa na changamoto kubwa ya visima visivyo endelevu ,visima ambayo vinakuwa na maji wakati wa mvua , msimu wa kiangazi vinakata maji.
" Visima ambavyo vilikuwa havikati maji yalikuwa ni maji ya chumvi sana , maji yenyewe yalikuwa machafu yanayotumiwa na binadamu na mifungo .
" Unachota maji wakati huohuo mifugo inaingia kunywa maji hayo na kuyachafua , inabidi mtu asubiri maji yatulie ndio achote.
" Hali hiyo ilisababisha mtu kutumia muda mwingi kusubiri ,matokeo yake anachelewa kurudi nyumbani kuendelea na majukumu yake, kulikuwa na changamoto sana ya kuchangia maji na mifugo" amesema Jackson.
Amesema kwamba wananchi wameupokea vizuri mradi huo ambao hauna changamoto tangu ulivyochimbwa hadi kukamilika na unawanufaisha wananchi.
" Kabla y mradi watu walitembea umbali mrefu kufuata maji visimani na kwenye vimto yalikuwa si safi lakini hiki kisima kimefunikwa tunapata maji kupitia bomba ambayo ni safi na salama hatuchangii na mifugo.
" Wananchi wameupokea vizuri mradi , maji yanatoka mengi hakuna tatizo. Mradi utakuwa na manufaa sana endapo maji hayatakuja kukauka, japo sidhani kama yatakauka kwasababu kuna kisima cha shule kina miaka mitano hakijawahi kukauka, kingine kipo karibu na mlima nacho hakijawahi kukauka" amesema Jackson.
Amesema kitendo cha watu kuchangia maji na mifugo iliwalazimu wanawake kuamka alfajiri saa kumi na moja kwenda kuchota maji.
" Waliamka alfajiri ili wakifika wachote maji kabla mifugo haijafika kuchafua maji maana ilipofika saa mbili asubuhi mifugo nayo inakwenda kunywa maji ili ikachunge" amesema .
Jackson Charles amesema wameanza kutumia maji hayo mwezi wa nne tangu , mwaka huu " Tunaipongeza kampuni ya WARACHA kutusogezea karibu huduma ya maji safi ambayo tunayapata bila gharama.
Mughosi Marare anayekadiliwa kuwa na umri zaidi ya miaka 60 amesema kabla ya visima hivyo walienda kuchota maji kwenye vijito na barabara wakati wa msimu wa mvua na msimu wa kiangazi maji yalikauka na kulazimika kuyatafuta mbali.
" Tulikuwa tunaenda kuchota maji kwenye vimto ,chini ya vidaraja ,tulikuwa tunachota maji kwenye barabara ambayo baada ya mvua yalikata .
" Jua likiwaka tunaenda kuyatafuta mbali mwendo wa masaa mawili . Maji hayo hayakuwa safi na salama ni maji ya kwenye visima vilivyo wazi machafu tuliyochangia na mifugo" amesema Mughosi.
Vanessa mkazi wa Kitongoji cha Nyamichere amesema" Tunashukuru kuletewa maji karibu ,mwanzoni tulikuwa na shida ya maji, sasa hivi hatuna shida ya maji hayakatiki , tunasema ahsante Mungu azidi kuwabariki" amesema Vanessa.
Vanessa mkazi wa Kitongoji cha Nyamichere, akionekana mwenye furaha baada ya kupata mradi wa maji ya bomba .
Luvian Nchagwa ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Nyamichere amesema tangu waanze kuchota maji ya bomba sasa anawahi kwenda shuleni kwakuwa maji yapo karibu na nyumbani na wanachota bure bila kulipa gharama yoyote.
Mwananchi wa Kitongoji cha Nyamanche amesema " Kwakweli tunashukuru tumepata maji ya bomba karibu, hatutahangaika tena kuchota maji na vibakuli kwenye visima . Haya maji yanatusaidia sana amesema Rhobi.
Sogore John ni msimamizi wa kisima kilichochimbwa Kitongoji cha Nyamanche ameiomba serikali ya Kijiji kuanza kumlipa fedha kwani amekuwa akilinda kisima bila kupewa malipo yoyote.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamanche Magweiga Chacha , amesema Kitongoji chake kina kaya 680 na kwamba anashukuru kwa msaada huo wa maji huku akiomba msaada wa visima vingine viwili ili viweze kukidhi mahitaji .
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamichere, Timasi Chacha amesema wamepokea mradi huo , wananchi wanatumia maji ya bomba huku akiomba waongezewe visima vingine viwili ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
" Wananchi wamefurahi sana WARACHA kuwachimbia visima , awali kisima kilikuwa uwanja wa ndege kilichokuwa kinatumiwa na vitongoji hivyo viwili lakini baada ya mgodi kuchukua maeneo, kisima hicho kikawa ndani ya mgodi na hivyo wananchi kukosa maji na kulazimika kutembea mbali kutafuta maji.
" Tunashukuru tumeweza kuchimbiwa visima vilivyochimbwa kwa mashine kubwa maji yamepatikana, wakatuwekea Sola, bomba na wakajengea na sasa maji hayo yanatumiwa na wakazi 970.
" Bado havijakidhi mahitaji kutokana na mazingira yetu haya ,upande wa mashariki hakuna kisima na Kitongoji chetu ni kikubwa, ningepata visima vingine viwili kama hivyo ngalau vingekidhi " amesema Timas.
Post a Comment