SHAIRI : UNAPANDA UTAVUNA
1. JEMA linakurudia,
Baya linakurudia,
Huu ujumbe sikia,
Unapanda utavuna.
2. Wafanya wafurahia,
Yale unajifanyia,
Mungu kumtumikia,
Unapanda utavuna.
3. Muda unautumia,
Mabaya kutumikia,
Yamkini utalia,
Unapanda utavuna.
4. Habari unasikia,
Mtu uweze mwambia,
Kimya unajikalia,
Unapanda utavuna.
5. Nguvu unazotumia,
Wengi kuwaumizia,
Kinyume zitakujia,
Unapanda utavuna.
6. Vibaya wamwangalia,
Mazuri yakimjia,
Nawe takugeukia,
Unapanda utavuna.
7. Mtu kakutumikia,
Ujira asubiria,
Wewe unamchunia,
Unapanda utavuna.
8. Mtu akuaminia,
Mali unamtunzia,
Wewe unaitumia,
Unapanda utavuna.
9. Kaka amekuchumbia,
Vyake umevitumia,
Meza wamgeuzia,
Unapanda utavuna.
10. Dada umemwahidia,
Ndoa mtajifungia,
Mitini unaingia,
Unapanda utavuna.
11. Mke akuaminia,
Mali anakutunzia,
Wewe nje wagawia,
Unapanda utavuna.
12. Mume anakufanyia,
Yote unahitajia,
Wewe wamdanganyia,
Unapanda utavuna.
13. Mzazi akufanyia,
Yote unahitajia,
Husomi unaishia,
Unapanda utavuna.
14. Hutaki kufikiria,
Mwenzio anaumia,
Kiburi wajimwagia,
Unapanda utavuna.
15. Bure wamshambulia,
Kosa hajakufanyia,
Sifa wamchafulia,
Unapanda utavuna.
16. Zengwe unamfanyia,
Ili aweze fulia,
Na chini kutumbukia,
Unapanda utavuna.
17. Haki unashikilia,
Chini waikanyagia,
Hutaki kumgawia,
Unapanda utavuna.
18. Hapo ulipofikia,
Watu uliwatumia,
Uko juu watulia,
Unapanda utavuna.
19. Wengine wanakujia,
Uweze wasaidia,
Vioo wawafungia,
Unapanda utavuna.
20. Wanalia wasikia,
Kimya wajinyamazia,
Sikio wawazibia,
Unapanda utavuna.
21. Neno linatuambia,
Tena huwa latimia,
Huna pa kujifichia,
Unapanda utavuna.
22. Fimbo unayotumia,
Wengine kuwachapia,
Kesho takugeukia,
Unapanda utavuna.
23. Muda unaotumia,
Wengine kubarikia,
Jua wajibarikia,
Unapanda utavuna.
24. Watu wanapokujia,
Na shida kukuambia,
Nawe ukapuuzia,
Unapanda utavuna.
25. Kikombe unatumia,
Ambacho unajutia,
Ni yako yakurudia,
Wavuna ulichopanda.
26. Kwato ulikanyagia,
Na wengine wakalia,
Hizo zitakurudia,
Unapanda utavuna.
27. Vema muda kutumia,
Wengine kubarikia,
Hapo wajibarikia,
Unapanda utavuna.
28. Hawa wawasaidia,
Mungu anafurahia,
Mema takurudishia,
Unapanda utavuna.
29. Mema yakutangulia,
Watu wakifurahia,
Baraka wajivutia,
Unapanda utavuna.
30. Mwongozo kujipatia,
Neno kufuatilia,
Mema unapalilia,
Unapanda utavuna.
31. Mabaya kutokujia,
Wewe wajiandalia,
Ni Neno linabakia,
Unapanda utavuna.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment