HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : SHIRIKI KUPIGA KURA

SERIKALI ni ya watu, na sisi wenyewe watu,

Huchaguliwa na watu, na kuongozwa na watu,

Hivyo ni wajibu wetu, kuchagua watu wetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Umri wako wa utu, hiyo kumi na nane tu,

Ukifika wewe mtu, hiyo ni sifa njema tu,

Wala usingoje kitu, jiandikishe wewe tu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Jinsi unapiga kura, ukiwachagua watu,

Ndivyo unafanya bora, kuwapata hawa wetu,

Watakaotunga sera, kwa maendeleo yetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Kumchagua Rais, huo ni wajibu wetu,

Wabunge wetu na sisi, pia ni kwa kura zetu,

Madiwani si mkosi, ni wa serikali zetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Pengine mpiga kura, kwamba una kadi zetu,

Umeshahamia Mara, wewe mpiga kura wetu,

Usifanye la kukera, jitambulishe wa kwetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Laboreshwa daftari, la wapiga kura wetu,

Kujipeleka vizuri, mpiga kura mwenzetu,

Hiyo ndiyo kwako siri, kuwachagua wenzetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Tena kwa umri wako, naona unafaa tu, 

Kutumia haki yako, gombea uongozi tu,

Cha muhimu sana kwako, uwe kwenye vyama vyetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Kugombea uongozi, kwenye hii nchi yetu,

Sifa zako ziwe wazi, zijulikane na watu,

Hapo yako moja kazi, kwenda kumwa sera tu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Kupiga kura vizuri, hawa wagombea wetu,

Wasikilize vizuri, wakimwaga sera kwetu,

Amani na siyo shari, tunataka nchi yetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Kama serikali yetu, kwa maendeleo yetu,

Kuchagua kazi yetu, siyo kumwachia mtu,

Wananchi twende zetu, tukapige kura zetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Tuombee nchi yetu, huu uchaguzi wetu,

Amani ibaki kwetu, pilikapilika zetu,

Kusiwepo kati yetu, kuleta ugomvi kwetu,

Ni mwaka wa uchaguzi, shiriki kupiga kura.

Mtunzi ni  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments