KARIBU UKWENI
WAKARIBISHWA ukweni, karibu wetu mgeni
Usijutie moyoni, hapa ni kwenu nyumbani
Utaishi kwa amani, bila shaka maishani
Karibu bibi harusi anapotokea mume
Wakwe wako wakarimu, pamoja na wifi zako
Kuwaheshimu muhimu, usiwe na chokochoko
Zingatia na nidhamu, usiwe kivyako vyako
Karibu bibi harusi anapotokea mume
Wakwe wako wathamini, wajali toka moyoni
Usiwe na kisirani, isimamie na dini,
Yaache ya mtaani, yaepuke kwa yakini,
Karibu bibi harusi anapotokea mume
Uchoyo usitamani, chakula kuficha ndani
Nakupa yangu maoni, yazingatie moyoni
Na kidogo kithamini, vya gharama sitamani,
Karibu bibi harusi anapotokea mume
Tano ni wa ukingoni, karibu sana ukweni
Sisi tutakuthamini, tutakutunza mwandani,
Tunakupenda jamani, tumekuweka moyoni,
Karibu bibi harusi anapotokea mume
Mtunzi ni Sirdody - Kilimanjaro,0762396923 au 0675654955
Post a Comment