WAKENYA HAYAWAHUSU, TUACHIENI WENYEWE
1. KIPI ninyi chawakera, nchi ya kwetu wenyewe,
Kelele zenu za chura, jipigieni wenyewe,
Rais wetu imara, tunamwamini wenyewe,
Hii Tanzania yetu, tuachieni wenyewe.
2. Mzozo wa Tundu Lissu, muachieni mwenyewe,
Wakenya hayawahusu, mwayachochea wenyewe,
Makali hayo ya kisu, mwajinolea wenyewe,
Hii Tanzania yetu, tuachieni wenyewe.
3. Wakenya amani yenu, mlivuruga wenyewe,
Huo ukorofi wenu, jifanyieni wenyewe,
Kwa hizo hasira zenu, jinsi mwajipa kiwewe,
Hii Tanzania yetu, tuachieni wenyewe.
4. Amani ya nchi yetu, tunayo sisi wenyewe,
Rais Samia wetu, twajivunia wenyewe,
Enyi majirani zetu, mbona mwampiga mawe,
Hii Tanzania yetu, tuachieni wenyewe.
5. Samia ni mama yenu, adhabu yenu mpewe,
Kwa hayo matusi yenu, aibu yenu wenyewe,
Maandamano ya kwenu, mlizoea wenyewe,
Hii Tanzania yetu, tuachieni wenyewe.
6. Hizi ni sheria zetu, tulipitisha wenyewe,
Kenya ni jirani zetu, jitathmini wenyewe,
Wakenya ni ndugu zetu, badilikeni wenyewe,
Hii Tanzania yetu, tuachieni wenyewe.
7. Msilete taharuki, tunasema mtutuwe,
Hatuitaki mikiki, mloileta wenyewe,
Ni kwenu hakushikiki, mrushianavyo mawe,
Hii Tanzania yetu, tuachieni wenyewe.
Mtunzi ni Paskalina Peter - Kishiri Mwanza - +255 768 861 084
Post a Comment