HEADER AD

HEADER AD

KITUO CHA AFYA MWABAYANDA ,MALAMPAKA VYAPOKEA GARI LA WAGONJWA


Na,Samwel Mwanga Maswa

WANANCHI wa Kata ya Malampaka na Kata ya Mwabayanda katika wilaya ya Maswa, mkoa wa Simiyu wameishukuru serikali kwa hatua ya kuwaletea magari ya kubebea wagonjwa ambayo yatahudumu kwenye  vituo hivyo.

Kituo cha afya cha Malampaka  kinahudumia wananchi zaidi ya 21,000 kutoka  katika wilaya hiyo pamoja na baadhi ya wananchi wa vijiji vya wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza.

       Gari la kubebea wagonjwa lililotolewa na Serikali katika kituo cha Afya Malampaka wilaya ya Maswa mkoa  wa Simiyu.

Pia kituo cha afya cha Mwabayanda kina hudumia zaidi ya wananchi 5,000 wa kata hiyo.

Makabidhiano ya magari hayo yamefanyika jana Mei 27,2025 kwa nyakati tofauti tofauti katika vituo hivyo yamefanywa na Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo,mbunge Ndaki amewataka wananchi na waganga wafawidhi wa vituo hivyo kuyatunza magari hayo na kuyawekea utaratibu mzuri wa matumizi.

     Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi wa mji wa Malampaka (hawapo pichani) mara baada ya kukabidhi gari la wagonjwa lililotolewa na Serikali katika kituo cha Afya Malampaka.

Amesema kuwa ni vizuri magari hayo yakaegeshwa katika maeneo ya vituo hivyo na siyo katika hospitali ya wilaya ya Maswa.

"Siku ya leo tunayofuraha kubwa ya kupata gari la wagonjwa katika kituo chetu cha Malampaka na Mwabayanda sina budi kuishukuru serikali kwa kutupatia magari hayo mapya kutokana na umuhimu wa vituo vyetu hivyo ambavyo vinahudumia maeneo mapana ya wilaya ya Maswa na nje ya mkoa wetu wa Simiyu,”amesema.

Khija Masunga ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bukigi kilichopo katika Kata ya Malampaka amesema kuwa msaada huo utawaondolea changamoto kubwa iliyowakabili kwa kipindi kirefu,hasa wanawake wajawazito na wagonjwa wengine ya kukosa usafiri wa haraka ili kuokoa maisha yao.

“Pindi wagonjwa walipokuwa wakipata rufaa ya matibabu zaidi kwenda hospitali ya wilaya ya Maswa iliyoko umbali wa kilomita 35 ilikuwa ni changamoto kwani kupata usafiri wa haraka ilikuwa ni shida,”amesema.

Amir Juma ambaye mkazi wa kijiji cha Mwabayanda ameishukuru serikali kwa kuwaletea gari hiyo,kwani itasaidia kuokoa maisha ya wananchi hasa wanawake.

      Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki(kulia)akikabidhi ufunguo wa gari la wagonjwa katika kituo cha Afya Mwabayanda.

“Siku za nyuma mke wa jirani yangu  alipata shida wakati wa kujifungua ilinilazimu nikodi pikipiki na ndio ilinisaidia kuokoa maisha yake kwenda hospitali ya wilaya ya Maswa,"amesema.

Naye Agnes James mkazi wa kijiji cha Mwatigi kata ya Malampaka anayepatiwa matibabu katika kituo hicho amesema anashukuru serikali  kwa uboreshwahaji wa huduma za afya kwa kuwaletea madaktari na wauguzi na leo wameletewa usafiri kwa wagonjwa na kusema gari hilo litasaidia sana kuokoa maisha ya wananchi.

Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Malampaka, Dk. Maiko Kienze ameeleza namna ambavyo huduma za upasuaji hasa kwa wakinamama wakati wa kujifungua wanavyopata changamoto ya namna ya kuwapeleka katika hospitali ya wilaya.

“Hapo awali gari hadi lije tulilisubiri umbali wa kilomita 35 kutoka wilaya ya Maswa hivyo ujio wa gari hilo la kubebea wagonjwa litasaidia kuokoa maisha ya wajawazito na shughuli za upasuaji endapo mgonjwa atahitaji huduma zaidi,”amesema.

Amesema kuwa gari hilo litaenda kuwa mwarobaini katika kuhakikisha linaokoa maisha ya wananchi hivyo litatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Magari hayo yamenunuliwa  na serikali kwa gharama ya Tsh. Milioni 200 kila moja ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za afya hapa nchini.

         Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki akiwa ndani ya gari la wagonjwa lililonunuliwa na serikali kwa ajili ya kituo cha Afya Malampaka wilaya ya Maswa.


No comments