KUMBE WAUAJI HUFA
WANGELIKUWA hawafi, wale wanaua watu,
Ngewapigia makofi, kile wanafanya kitu,
Kwamba wao ukorofi, kwao haupati kitu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Uhai wanakatisha, asiye na kosa mtu,
Au mtu kukausha, hata akifanya kitu,
Nyoyo wazifurahisha, ni kama wataishi tu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Mtu ana mali zake, amezidunduliza tu,
Ale na famile yake, hana ugomvi na mtu,
Nyie mwavamia kwake, kuiba na kuua tu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Vibaka nyie njiani, mnaovizia watu,
Watu waenda nyumbani, wamebeba vyao vitu,
Mnawachoma kooni, mwatoka na vyao vitu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Sasa kama kitokea, nyie kubambwa na watu,
Kile kinaendelea, japokuwa siyo kwatu,
Kule mnaelekea, ni kwenye kifo kile tu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Pengine watu vitani, wapiganapigana tu,
Wengine wapigwa chini, na wengine washindi tu,
Ila kwa wote mwishoni, ni kwenda kaburini tu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Mtaje yeyote yule, aloua sana watu,
Naye kifo kilekile, ndicho alikipata tu,
Aenda na dhambi tele, za mauaji ya watu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Kama wewe muuaji, unauaua watu,
Kisu chako si mtaji, kwamba utapata kitu,
Wala hutavikwa taji, hata utumwe na mtu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Geuza akili yako, kupenda kuua watu,
Upendavyo mwili wako, vivyo uwapende watu,
Hao viumbe wenzako, twaishi mara moja tu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Natamani wauaji, wajue watakufa tu,
Waache wawe wachaji, wamjue Mungu wetu,
Neema yake mtaji, waishi vema na watu,
Kumbe wauaji hufa, sasa kwanini waua?
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.comKUMBE WAUAJI HUFA
Post a Comment