HEADER AD

HEADER AD

KUSAKA NDOTO ZILIKO


SIKILIZA moyo wako, sizimishe ndoto zako,

Hiyo ni hatima yako, na utimilifu wako,

Tena ni mwongozo wako, na utoshelevu wako,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Huwa ninaguswa sana, mtu mmoja aliko,

Afanyaye mema sana, kutuletea mwamko,

Dunia yafana sana, na kukileta kicheko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Yesu nisipomtaja, sitafika kwingineko,

Alifanya yenye haja, yasemavyo maandiko,

Anatuweka pamoja, tuje tufike aliko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Wapo mmoja mmoja, maarufu sana huko,

Kwa mema siyo vioja, cheki cheki maandiko,

Sifa kubwa kwao moja, kusaka ndoto ziliko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Nyerere huko aliko, alofanya kwetu yako,

Hebu ujipe mwaliko, soma yake maandiko,

Uhuru haukuweko, lakini kwa sasa uko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Huko Kaunda aliko, ingawa yeye hayuko,

Histori yake iko, kusaka uhuru yuko,

Ukombozi pia yuko, ingawa sasa hayuko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Kwa Kenya Kenyatta yuko, siyo huyu aliyeko,

Uhuru lisaka huko, wakakipata kicheko,

Sasa nchi Kenya iko, wanachaguana huko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Maarufu sana hao, ni watu walikuweko,

Na teknolojia hao, na kwao haikuwako,

Pia hata pesa hao, mwanzoni hazikuwako,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Watu bora pia pesa, teknoloji ni yako,

Wataipata fursa, kubuni kwajili yako,

Maishani utatesa, na kufanya mambo yako,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Huo ndio uvumbuzi, elimu ya maandiko,

Sikia utandawazi, viwili lake tambiko,

Dunia kijiji wazi, katika kizazi tuko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Upate watu wazuri, na hiyo Tehama yako,

Una mtaji mzuri, kuyafanya mambo yako,

Utapeta siyo siri, kwa hii dunia yako,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Maarufu wa zamani, ambao sasa hawako,

Ni mapenzi na imani, vilivyowapa mwamko,

Kutikisa duniani, twawakumbuka waliko,

Hii teknolojia, watu pesa mambo yote.


Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments