HEADER AD

HEADER AD

RC PWANI ASEMA SERIKALI IMEJIPANGA KUENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA UWEKEZAJI


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amefungua mkutano wa Baraza la Biashara la mkoa wa Pwani huku akiwahakikishia wawekezaji wakimataifa na  wafanyabiashara wa ndani kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuboresha miundombinu ya uwekezaji.

Kunenge,ametoa kauli hiyo Mei 22, 2025 katika mkutano uliofanyika Mjini Kibaha na  kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa sekta binafsi, wakuu wa taasisi za Umma, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Maafisa biashara wa Halmashauri.

Amesema kuwa mkoa wa Pwani unafursa nyingi za uwekezaji ikiwemo katika Viwanda,Kilimo ,Ufugaji ,Uvuvi ,Utalii na hata katika biashara mbalimbali ambapo ametaka wawekezaji kuja kwa wingi kwakuwa Serikali tayari imeweka mazingira rafiki kwao.

        Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akifungua mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Pwani lililofanyika Mei 22,2025 Mjini Kibaha.

Amesema kuwa, Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanyakazi kubwa ya kuboresha mazingira ya biashara nchini na kwamba hatahivyo bado juhudi hizo zinaendelea.

Kunenge,amesema anafahamu kuwa changamoto kubwa ni ardhi,Maji ya kutosha na Nishati lakini tayari ufumbuzi wa changamoto hizo unaendelea kufanyika kwa kuweka mikakati mbalimbali.

Amesema kuwa, kuhusu umeme tayari Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere limekamilika na linazalisha zaidi ya Megawati 2000 lakini bado vitu vidogo kukamilisha japo kwasasa Pwani inapata umeme wa kutosha wa Megawati 140 tofauti na miaka ya nyuma iliyokuwa ikipata Megawati 110.

Kuhusu ardhi amesema kuwa , wawekezaji wengi wanakuja Pwani lakini wananunua ardhi kwa gharama kubwa lakini kwa kutambua hilo tayari Serikali imejipanga kuweka maeneo maalum ya uwekezaji ambayo mwekezaji atapata kwa gharama nafuu.

Amesema kuwa,kuwepo kwa eneo hilo itasaidia kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kufanya shughuli zao kirahisi na kwamba mtu ambaye hatanunua eneo hilo atanyimwa kibali cha Uwekezaji.



"Serikali imejipanga kuweka maeneo  maalum ya uwekezaji ambapo itamlazimu mwekezaji yeyote kununua eneo hilo na endapo akinunua maeneo mengine ambayo hayajapimwa kwa ajili ya  Uwekezaji wa Viwanda atanyimwa kibali ,"amesema Kunenge 

 Ametaka wawekezaji wanaokuja Pwani wahakikishe wanafungua ofisi zao Kuu ndani ya Mkoa ili kufanya mkoa uzidi kukua kiuchumi na ongezeko la mapato kwani kwasasa Makao Makuu ya viwanda vingi vipo Jijini Dar es Salaam na hivyo kupelekea Pwani kukosa mapato.

Pamoja na mambo mengine lakini pia Kunenge amemshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa ya kuiongoza nchini na kuboresha mazingira ya uwekezaji na mazingira ya biashara nchini huku akisema tangu Rais Samia aingie madarakani Pwani imejenga Viwanda 131 na kati ya hivyo 78 ni Viwanda vikubwa.

Amesema kwa sasa vikao vya mabaraza ya biashara yanaanzia ngazi ya Wilaya jambo ambalo linasaidia kuinua fursa za biashara pamoja na utatuzi wa kero zinazowakabili.

    Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa wa Pwani  na wadau wa biashara katika kikao cha baraza la biashara Mkoa leo Mei 22,2025

" Mabaraza yanaanzia huko chini ili kuhakikisha tunaboresha na kuwawezesha wazawa na wafanyabiashara waweze kukua na kuanzisha viwanda vyao na hili limefanyika kupitia Rais Samia",amesema Kunenge 

Hatahivyo, Kunenge amewapongeza Wakurugenzi kwa makusanyo mazuri ya mapato na kwamba awamu iliyopita Mkoa wa Pwani ulikuwa wa pili ukitanguliwa na mkoa wa Dar es Salaam.

Katibu wa Baraza la Biashara la Taifa Dkt.George Wanga ,ametaja baadhi ya vigezo vya ushindani wakibiashara vinavyoweza kuupa Mkoa ushindi kuwa ni kuhakikisha kila kiwanda kinakuwa na makao yake ndani ya mkoa .

            atibu wa Baraza la Biashara la Taifa Dkt.George Wanga akizungumza katika mkutano wa baraza la biashara la Mkoa wa Pwani

Wanga , amesema kuwepo kwa ofisi hizo kunasaidia taasisi wezeshi kama vile NBS,TBS na zingine kupata takwimu sahihi za uzalishaji na hata makusanyo ya mapato.

Amesema ,vigezo vingine ni kuimarisha vivutio,kuongoza utatuzi wa changamoto za kuimarisha mazingira ya biashara,kupunguza gharama za kuanzisha biashara, kupunguza gharama za kukidhi matakwa ya kisheria pamoja na kuboresha na kuimarisha muelekeo na msimamo wa kisera na mkakati wa kuvutia zaidi wafanyabiashara.

Amesema, kingine ni kuweka sera , mikakati na mafunzo ya kuendeleza biashara na wafanyabiashara wa sekta binafsi, kuimarisha na kuongeza ufanisi wa utatuzi wa kibiashara,kurahisisha upatikanaji wa ardhi na maeneo ya biashara na Uwekezaji na kupunguza gharama zisizo rasmi  kibiashara.

Kwa upande wake mwenyekiti wa taasisi ya chemba ya biashara Mkoa wa Pwani (TCCIA) Mkoa wa Pwani Said Mfinanga ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara huku akiomba kuhakikisha inapunguza gharaza za upatikanaji wa ardhi kwa wafanyabiashara wazawa.

     Mwenyekiti wa chemba ya biashara Mkoa wa Pwani (TCCIA) Said Mfinanga


No comments