TUJIEPUSHE NA MIRUNGI

MIRUNGI ni ufakiri, kailaani Manani,
Kutafuna si vizuri, ina madhara mwilini,
Kutokulala vizuri, usingizi mashakani,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Kupata chuo kigumu, mirungi yake athari,
Hali inakuwa ngumu, na uchumi huathiri,
Kuzingatia muhimu, kutafuna si vizuri,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Mlaji huathirika, kiuchumi anashuka,
Ninayosema hakika, mwisho anafilisika,
Wengi wameathirika, wapo waliyoumbuka,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Kondoa ni kituoni, mahala pakufikia,
Inaliwa siutani, mifano tunayo pia,
Faida yake ni nini, tuache hiyo tabia,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Elimu nawapatia, mirungi sumu mwilini,
Vijana nawahusia, na hilo jiepusheni,
Ushauri nautoa, bila ya chuki moyoni,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Wake zetu walalama, nguvu zimeshapungua,
Kwa kweli siyo salama, hamu tunawaachia,
Wanaitaka heshima, ya ndoa kufurahia,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Madeni yamezidia, kiasi vyombo kuuza,
Na nyama imepotea, nyumbani ninawajuza,
Watoto walia njaa, chakula unakiuza,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Mwishoni nimefikia, shairi ninalitoa,
Vizuri kuzingatia, ushauri kuchukua,
Mengi nimeelezea, mazuri na yenye nia,
Tuzilinde afya zetu mirungi tusitafune.
Mtunzi wa Shairi ni Sirdody-Kilimanjaro Tanzania- 0675654955 , 0762396923
Post a Comment