MOTO, UVAMIZII WATISHIA URITHI WA DUNIA NCHINI
Na Samwel Mwanga, Serengeti
MAJANGA ya moto na uvamizi katika maeneo ya hifadhi za Taifa yameendelea kuwa tishio kwa maeneo ya urithi wa Dunia na vituo vya urithi wa Taifa hapa nchini huku wataalamu wakitaka hatua za haraka zichukuliwe ili kuyalinda maeneo hayo dhidi ya uharibifu wa kudumu.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ( TANAPA) Stephano Msumi amesema hayo Mei 4, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ndani ya hifadhi juu ya kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya urithi wa dunia, Afrika isemayo 'Majanga na migogoro ni tishio kwa urithi wa dunia'.
Amesema kuwa maeneo kama hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro na mapango ya Kondoa yanakabiliwa na changamoto za moto wa porini na uvamizi wa binadamu kwa ajili ya kilimo, uchomaji mkaa na makazi yasiyo rasmi.
“Moto na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ni tishio kubwa kwa urithi wetu wa dunia,ikiwa hatutachukua hatua sasa, tunaweza kupoteza maeneo haya,” amesema.
Amesema kuwa ni vizuri wataalam wa mazingira kuweka mipango madhubuti ya usimamizi wa majanga, ikiwemo elimu kwa jamii, uwekaji wa mipaka ya hifadhi na vituo vyote vya urithi wa dunia, uboreshaji wa vifaa vya kuzima moto, na ushirikishwaji wa wanavijiji katika ulinzi wa maeneo haya muhimu.
Meneja wa kituo cha michoro ya mapango ya Kondoa Irangi , Zuberi Mabiye, amesema kuwa baadhi ya maeneo hayo yako hatarini kupoteza michoro ya miambani inayodaiwa kuwa na zaidi ya miaka 2,000 kutokana na joto kali na hatari ya moto wa msituni.
Meneja wa kituo cha michoro ya Mapango Kondoa,Zuberi Mabiye(kulia)akizungumza na Waandishi wa habari juu ya hatari ya moto wa mstuni unaotishia kutoweka kwa urithi huo wa dunia.“Urithi huu ni hazina ya taifa,tunapaswa kuwekeza katika ulinzi wake kwa sasa ili vizazi vijavyo vinufaike,”amesema.
Naye Mkurugenzi wa idara ya elimu tafiti na uwekezaji, Mamlaka ya uhifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar, ambao ni sehemu ya Urithi wa Dunia, Asha Hassan, amesema kuwa kumekuwa na msongamano wa makazi ya watu waliovamia eneo hilo.
Pia amesema kuwa kuwepo kwa wafanyabiashara ndogondogo katika eneo la mji mkongwe ambao wamevamia inaweza kusababisha janga kubwa la kihistoria kutoweka la mji huo.
“Katika mji mkongwe wa Zanzibar pale kuna msongamano wa makazi pamoja na wafanyabiashara katika eneo hilo la kihistoria hilo ni janga ambalo linaweza kusababisha kutoweka kwa urithi wa dunia hivyo kuna mipango inayofanywa na serikali ya mapinduzi Zanzibar kutafuata eneo na kuwahamishia wafanyabiashara hao.
“Urithi huu si wa kizazi kimoja, ni hazina ya taifa na dunia. Tukichelewa kuchukua hatua, tunaweza kupoteza historia isiyoweza kurudi tena,” amesema.
Kilele cha Maadhimisho ya siku ya urithi wa dunia, Afrika kitafanyika Mei 5,2025 mjini Mugumu wilaya ya Serengeti na mgeni Rasmi anatarajia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara,Kanali Evance Ntambi.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Stephano Msumi wakati akielezea maadhimisho ya siku ya urithi wa dunia,Afrika ndani ya hifadhi ya Serengeti.
Post a Comment