SERIKALI NA UTEKELEZAJI MIRADI YA KIMKAKATI SHINYANGA

>> Bilioni 17 kukuza kilimo cha pamba
>> Bilioni 4 zaboresha miundombinu
>>Bilioni 44.8 kugharimu ujenzi wa uwanja wa ndege
Na Neema Andrew, Shinyanga
KATIKA kudhihirisha dhamira ya kuijenga Tanzania mpya, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kipekee katika kuhakikisha kila mkoa unashiriki kikamilifu katika safari ya maendeleo.
Katika mkoa wa Shinyanga, juhudi hizo zimejidhihirisha kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, huku wananchi wakishuhudia mabadiliko yanayoleta matumaini mapya.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari , Uatamaduni , Sanaa na Michezo ambaye pia ni msemaji mkuu wa Serikali, Greyson Msigwa akiwa katika kijiji cha Sayu, Kata ya Pandagichiza amesema kuwa Serikali imewekeza Tsh. Bilioni 17 katika kukuza kilimo cha pamba.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari , Uatamaduni , Sanaa na Michezo ambaye pia ni msemaji mkuu wa Serikali, Greyson Msigwa akizungumza .
Amesema uwekezaji huo unahusisha upatikanaji wa zana za kisasa, mafunzo kwa maafisa ugani na utoaji wa pikipiki kwa urahisi wa kuwafikia wakulima vijijini.
Msigwa amesisitiza kuwa kwa kutumia mbinu za kitaalamu na teknolojia ya kisasa, wakulima wanaweza kuongeza tija kutoka kilo 300 hadi kilo 1,200 kwa ekari.
" Hii ni fursa ya kipekee ya kiuchumi kwa wakulima wa Shinyanga, hususan vijana na wanawake, wanaoanza kujitokeza katika sekta ya kilimo kama njia ya kujikwamua kiuchumi" amesema Msigwa.
Msemaji mkuu wa serikali akiwa ametembelea shule ya sekondari ya Wasichana Shinyanga, amesema katika upande wa elimu zaidi ya Tsh. Bilioni 4 zimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa.
" Uwekezaji huu unalenga kuweka mazingira salama, rafiki na ya kuhamasisha ufaulu kwa mtoto wa kike, hasa katika masomo ya sayansi. Hii ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wasichana wanapata nafasi sawa katika elimu ya juu na fursa za ajira za kitaalamu" amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa katika sekta ya usafiri, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga unaendelea kwa kasi, na kwamba kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025 kwa gharama ya Tsh. Bilioni 44.8.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutafungua milango ya biashara na kuharakisha mawasiliano kati ya mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.
Post a Comment