HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : MATATU NINAKUOMBA


UMEPATA mchumba, muingie kwenye ndoa,

Matatu ninakuomba, chunguza asije boa,

Ukakuta ni mtumba, wadudu weshatoboa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Ngoma kwako ukiwamba, ukubali yuko poa,

Kama wimbo ukiimba, maoni aweze toa,

Si wa kukuchimbachimba, au wa kukuzodoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Kwako asiwe ni simba, amani anaondoa,

Awe wewe ukiyumba, hofu yote akutoa,

Pamoja muweze imba, nyimbo hata kusogoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Asiwe anayetamba, jinsi pesa akutoa,

Awe anapenda shamba, pesa wanakozitoa,

Si kukufunga kamba, kwingine akijojoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Mchakarikaji mwamba, bora jasho akitoa,

Huyo akiwa kunyumba, njaa ataiondoa,

Mwaweza kukaa chemba, na mipango mkatoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Kama kwako ni mchumba, uone anajitoa,

Nauli kuombaomba, huyo aweza kuboa,

Kukutoa anaomba, nauli ashindwa toa?

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Maamuzi ya kuyumba, kwako anajiondoa,

Ndugu zake wa kunyumba, hadi wanapokohoa,

Homa yaweza kukumba, maamuzi akitoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Nawe aweze kutamba, wala si kujiondoa,

Hata kukiwa na njemba, kwako aweze jitoa,

Ni wapenzi si wajomba, kwako aweze jitoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Nawe usijekuyumba, mwili wako kuutoa,

Kesho abaki kuchamba, asali akishatoa,

Au ubaki na mimba, yeye akijiondoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Kwani kumcha Muumba, huko ndiko kujitoa,

Huyu aliyetuumba, hekima kwetu atoa,

Mengine yakitukumba, atupa kuyaondoa,

Awe anamcha Mungu, Muumba anayeishi.


Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments