MTUMWA…UNAFANYA KAMA NDIO
KAMA wewe ni mtumwa, kazi ni kutumwatumwa,
Akili ni za kutumwa, na kazi ni za kutumwa,
Unaishi unaumwa, kwa jinsi unavyogemwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Ni mzima hujaumwa, kutenda kitu watumwa,
Si kwa akili kusomwa, kifuatacho kulimwa,
Mbaya sana utumwa, akili zote wagemwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Kuna watu walitumwa, kisha huko wakafumwa,
Kilichofwata kulimwa, na hukumu zikasomwa,
Kusemwa walivyotumwa, hawawezi ni watumwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Alomchinja Yohana, na Herode alitumwa,
Vipi yeye aliona, kufanya alichotumwa,
Hivi huyo kesi ana, au aachwa mtumwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Teseka huko mtumwa, uzidi kutumwatumwa,
Ukikamatwa mtumwa, tonge ndipo utakwamwa,
Na sheria utagemwa, ndivyo utakavyosemwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Kazi za kutumwatumwa, kweli mkubwa utumwa,
Ukishakuwa mtumwa, vipi usitake tumwa,
Mwenye waweza kulimwa, na hitima ikasomwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Mungu akusaidie, mfanyakazi mtumwa,
Tena akuepushie, mitihani ya kutumwa,
Kwenye haki usalie, na mtu usijesemwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Njaa chanzo cha kutumwa, japo lifutwa utumwa,
Bado tunatumwatumwa, ubaya wema twatumwa,
Maisha yetu kutumwa, hadi dunia kutemwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Kama hutaki kutumwa, ajira usijesemwa,
Akili yako kutumwa, bora kuliko utumwa,
Na mtu huwezi semwa, vile wewe si mtumwa,
Hata ukijua siyo, unafanya kama ndio.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment