Home
/
HABARI KITAIFA
/
SERIKALI : UTOAJI LESENI KWA VIJANA UTAPUNGUZA ATHARI ZA MAHUSIANO KATI YA VIJIJI , MGODI WA NORTH MARA
SERIKALI : UTOAJI LESENI KWA VIJANA UTAPUNGUZA ATHARI ZA MAHUSIANO KATI YA VIJIJI , MGODI WA NORTH MARA
>> Vikundi 48 vya vijana wanaozunguka mgodi wa Barrick North Mara vyapewa leseni za uchimbaji
>> Waziri Mavunde asema ahadi imetekelezwa
Na Dinna Maningo, Tarime
SERIKALI imesema kwamba utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini ya dhahabu, kwa vijana wanaozunguka mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilaya ya Tarime, mkoani Mara, zitasaidia kupunguza athari za kila mara za mahusiano zilizokuwa zinajitokeza kati ya jamii, mgodi na Serikali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde akiwa Nyamongo, Mei , 03, 2025 wakati akikabidhi leseni za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa vikundi 48 vya vijana wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara, ili kujiinua kiuchumi.
" Serikali na mgodi wa Barrick North Mara tulikaa tukaona ni njia gani bora iweze kutumika ili kuweza kupunguza athari za kila siku za mahusiano zilizokuwa zinajitokeza kati ya jamii ya vijiji vinavyozunguka mgodi, mgodi na Serikali.
" Naupongeza mgodi wa North Mara kwa hatua nzuri mlioifikia, tulizungumza kwa pamoja na kuelewana vizuri namna ya kujenga mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka .
" Ninyi watu wa mgodi mnafahamu kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa shughuli za madini duniani ni muhimu sana wananchi waone tija uwepo wa mgodi" amesema Waziri Mavunde.
Waziri huyo amesema mradi huo wa vijana ni wa kwanza nchini Tanzania na katika Bara la Afrika mradi wa mgodi kufanya mahusiano makubwa na jamii hasa vijana .
" Vijana mnaingia katika historia ndio kundi la kwanza ambalo tumeweka utaratibu wa kuweza kufanya kazi vizuri na mgodi na Serikali ili kuweza kuwa na manufaa ambayo mwisho wa siku yataweza kuwajenga kiuchumi na kubadilisha maisha .
" Niipongeze wizara kupitia ofisi ya mtendaji wa tume, serikali imetoka leseni zaidi ya 39 pamoja na leseni za mgodi . Lakini nilielekeza leseni zote ambazo hazifanyiwi kazi naendelea kuzifuta na tutazigawa kwenye makundi ya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu, Wazee na wababa." Amesema.
Amesema Leseni na maombi 2,648 zimefutwa ili kuwezesha watanzania kushiriki kwenye uchumi sekta ya madini kwani watu wamekuwa wakishikilia maeneo makubwa lakini hawayafanyii kazi na kuwafanya watu wengine kukosa shughuli za kufanya.
" Wapo watu wenye leseni zilizokuwa na ukubwa wa mikoa minne kama mkoa wa Kilimanjaro anamiliki mtu mmoja. Mwingine tulimfutia maombi yenye ukubwa wa mikoa 11 kama mkoa wa Dar es Salaam anamiliki mtu mmoja, nimefuta zote " amesema Mavunde.
Ameongeza kuwa zoezi la utoaji leseni kwa vijana ni ahadi yake aliyoiahidi kwa wananchi akiwa Nyamongo , Mei, 05, 2014 ambapo pamoja na mambo mengine changamoto kubwa ilikuwa mahusiano.
" Nilipokuja hapa Nyamongo mkutano ulikuwa mgumu sana, ndio mara ya kwanza kutoshangiliwa wala kupigiwa makofi . Niliahidi katika kutatua changamoto ya mahusiano tutakaa na mgodi tupate leseni. Leo tuko hapa kwasababu ya maridhiano na mgodi.
" Naamini na migodi mingine Tanzania itaiga Barrick North Mara kutenga maeneo kwa ajili ya jamii inayowazunguka. Hao ni wananchi wana mioyo ya nyama ,wana matamanio , wana hisia .
" Kibinadamu wakiona maroli ya mchanga yanapita hapa , ndege zinapita kubeba dhahabu wanaishia kutazama kwa macho hawajisikii vyema wanatamani na wao wanufaike " amesema.
Waziri Mavunde amesema mradi huo utasaidia kupunguza changamoto za ajira kwa vijana , itasaidia kuhakikisha vijana wanapata fursa ili maisha yao yaendelee .
Amesema walezi wa mradi huo wa kwanza ni mkuu wa mkoa wa Mara, Meneja wa Barrick na Waziri wa madini na kwamba Benki ya dunia ,Baraza la Dhahabu Duniani zimeonesha utayari kushirikiana na vijana kuendeleza mradi huo.
"Zaidi ya watu 2000 wanakwenda kunufaika katika awamu ya kwanza na itaendelea katika awamu zingine .Mradi mkubwa unaowalenga, vijana , akina mama na walemavu, ni mradi wa kwanza wilaya ya Tarime.
" Waliohisi kuwa mradi huu ni wa kisiasa kwamba ni mwaka wa uchaguzi kuwa watu wanataka kuweka mazingira ya Waitara na CCM kwa ajili ya uchaguzi hao wamepitwa na fursa.
" Kampuni ya miamba wapo tayari kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiufundi kwa ajili ya uchimbaji . Mwakilishi wa nchi za umoja wa Ulaya nao wapo tayari kuungana nasi katika mradi huu.
" Niwaombe vijana twendeni tukafanye kazi ili mradi ulete matokeo chanya katika uchumi wetu na nchi ya Tanzania. Pia nimeunda kamati ya watu 6 watakamilisha kazi yao tarehe 15, 5, 2025 ya kuja kushauri serikali namna ya kuwezesha wachimbaji watanzania hasa sekta ya madini" amesema Waziri Mavunde.
Kauli ya Afisa Madini Mara
Afisa Madini Mkazi mkoa Mara, Amini Msuya amesema hadi kufikia siku hiyo ya utoaji leseni kwa awamu ya kwanza, vikundi vya vijana 48 vyenye jumla ya watu 1,736 vimesajiliwa , ambao wanaingia moja kwa moja kama wamiliki wa mradi.
"Tulibainisha maeneo ambayo yameingizwa kwenye mradi, tumepata maeneo kutoka sehemu mbili, mgodi ulitoa leseni nne za utafiti zinazotoa leseni nyingi za uchimbaji mdogo na kuzigawa kwenye mradi, na serikali ilitoa leseni 39 za uchimbaji mdogo na kuzigawa kwenye mradi.
" Leseni tutakazozitoa kwa awamu ya kwanza zipo leseni 106 zitatolewa kwenye maeneo husika, na leseni 96 ni za vikundi na leseni 48 hizi ni leseni moja moja kutoka kwa kila wilaya , kila kikundi kitachukua leseni 2 .
" Leseni kumi zimetengwa ila bado hazijatolewa kwa ajili ya kuwagawia vijana watakaoandikwa kwenye vijiji tunakopeleka leseni zingine " amesema Msuya.
Ushauri wa RC Mara
Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema utoaji wa leseni kwa vikundi vya vijana ilikuwa ni njozi ya mkoa huo huku akiwasisitiza vijana kutumia fursa hiyo kujiinua kiuchumi.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa vijana wa madini.
" Tuliona bila vijana hawa kuwa na kazi ambayo itawapatia kipato halali hususani ya machimbo tuliona bado tutaendelea kuwa na changamoto .
" Leo nafarijika kwa jambo hili la kuwapatia vijana leseni za uchimbaji wakachimbe wapate fedha. Vijana tumieni fursa hii adhimu mmeipata , mkiitumia vizuri hakika mtatoboa maisha " amesema RC Evans.
Msisitizo wa Barrick North Mara
Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko ameipongeza kamati iliyoundwa kwa ajili ya kushughulikia leseni kwa vijana.
Amesisitiza ni furaha kwa mgodi wa Barrick kuona vijana wakipata shughuli halali za kufanya na kufuata sheria za nchi, taratibu na miongozi inayotolewa na serikali ili wote waweze kujenga jamii inayoheshimu utawala na maadili.
" Ni imani yetu safari tunayoianza leo kupitia leseni hizi itawafanya vijana kuwa na mawazo chanya katika maendeleo kwa kufanya kazi halali ambazo zitawanufaisha kiuchumi " amesema Apolinary.
Mbunge aomba utafiti wa kina
Mbunge wa Jimbo la Tarime , Mwita Waitara kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), ameiomba serikali kufanya tafiti za kina katika maeneo ambayo leseni zimetolewa kwa kina huku akiomba vijana wasaidiwe mitaji ili waweze kumudu shughuli zao za uchimbaji.
" Waziri umesema hawa vijana utawalea isije ikatokea hawa vijana wakapewa maeneo ambayo hayana kitu. Mashimo yote na leseni watakazopewa zifanyiwe utafiti wa kutosha .
" Pia vijana wengi ni masikini hawana mtaji na wanataka kuanza uchimbaji tunaomba vijana wasaidiwe mitaji , mashine za uchimbaji " amesema Waitara.
Madiwani wahimiza vijana
Diwani wa Kata ya Kemambo Rashid Bogomba kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), amesema utoaji wa leseni ni mkombozi wa vijana huku akiwaomba kutumia vyema fursa hiyo kujipatia mapato yatakayosaidia jamii.
Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye kupitia CCM amesema kilimo cha wananchi Nyamongo ni dhahabu na kwamba walikuwa hawana sehemu ya kwenda kulima , hivyo kitendo cha serikali na mgodi kutoa leseni kitawainua vijana kiuchumi.
Amewaomba vijana kushirikiana kwa umoja katika vikundi vyao vya uchimbaji kwani wakiwa wamoja watafika mbali.
Bhoke Mwita mkazi wa kijiji cha Nyangoto amesema moja ya sababu iliyosababisha wananchi kuvamia mgodi ni kutokuwa na maeneo ya kuchimba dhahabu na kwamba utoaji wa leseni kwa vijana utasaidia kuondoa vitendo vya vijana kuvamia mgodi.
Katika uzinduzi huo wa mradi wa wachimbaji wameshiriki pia viongozi mbalimbali ambao ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Patrick Chandi, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tarime Daud Ngicho, mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele, Meneja Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara Francis Uhadi, watendaji wa Kata, vijiji, wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka mgodi na wananchi.
Post a Comment