MWENYEKITI : HAKUNA ATAKAYEBOMOA NYUMBA ZA WANANCHI
Na Gustaphu Haule, Pwani
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Kwakibosha katika Kata ya Mapinga Bagamoyo Mkoani Pwani Shaban Athumani , amewatoa wasiwasi wakazi wa eneo hilo kuwa hakuna mtu wa kuwavunjia nyumba zao.
Amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni sikivu na haipo tayari kuona watu wake wanadhulumiwa haki zao.
Athumani amewaambia wananchi hao kuwa kama kuna mtu anataka kuvunja nyumba zao na kupora ardhi kwa utapeli basi kamwe haitowezekana na kwamba amewatahadhalisha matapeli hao kukaa mbali na eneo hilo kwakuwa Serikali haitaweza kuvumilia kuona watu wake wakiteseka.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwakibosha Kata ya Mapinga Bagamoyo Mkoani Pwani Shaban Athumani akizungumza na Waandishi wa habari Mei 20,2025 kuhusu mgogoro wa ardhi unaoendelea katika eneo hilo.Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika mkutano maalum uliofanyika katika eneo la Kwakibosha Mei 20, 2025 uliowashirikisha Wananchi hao ikiwa ni sehemu ya kuwaondoa Wananchi taharuki iliyosambaa kuwa yupo mtu anataka kuwavunjia nyumba Wananchi hao.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, amesema yupo mtu anayejulikana kwa jina la Peter Junior ambaye amezua taharuki kwa Wananchi wa eneo hilo kuwa anataka kuvunja nyumba za wakazi hao kwakuwa eneo hilo ni mali yake.
Athumani amesema kuwa kinachosikitisha zaidi ni kuona Peter Junior kaenda Mahakamani kumshtaki Peter Maro kwa madai ndiye aliyechukua eneo hilo wakati huyo Peter Maro si Mkazi wa eneo hilo ,wala hajulikani katika eneo hilo na hajawai kumiliki kipande cha ardhi Kitongojini hapo.
Wananchi wa Kitongoji cha Kwakibosha wakiwa katika mkutano maalum na Mwenyekiti wao kuhusu taharuki ya kuvunjiwa nyumba zao na kuporwa mashamba yao."Huyu Peter Junior amezua taharuki kubwa katika Kitongoji hiki na kuwafanya Wananchi kukosa amani na kuanza kuhaha lakini namuambia Peter Junior hapa hana eneo kwani hata huyo aliyemshtaki hajawai kumiliki kipande cha ardhi hapa, kwahiyo amtafute huyo Peter Maro akamuoneshe hiyo ardhi yake lakini sio kuja hapa na kuanza kuwasumbua Wananchi bila sababu,"amesema Athumani.
Amesema kuwa ni kweli Peter Junior alikwenda Mahakamani kumshtaki Peter Maro ambaye anadai alivamia eneo lake lakini tuzo ya Mahakama imetoka na kumtaka Peter Maro aondoke lakini huyo Peter Maro hana ardhi hapa na wala hajulikani sasa jambo ambalo linashangaza kuona anataka kuwavunjia wananchi nyumba zao.
Athumani amesema kuwa Peter Junior miaka miwili iliyopita alikwenda katika eneo hilo na kuvunja nyumba 12 za Wananchi na sasa anataka kurudi tena kwa kuvunja nyumba 120 zenye Wananchi zaidi ya 300 akitaka waondoke lakini uchunguzi wakina umefanyika na vielelezo vya kisheria vimepitiwa na kubainika kuwa Peter Junior hana ardhi katika Kitongoji hicho.
Wananchi wa Kitongoji cha Kwakibosha wakiwa katika mkutano maalum wa kujadili ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi katika Kitongoji hicho Mei 20,2025."Hili eneo la Kwakibosha linaekari 17 ambalo Wananchi wamejenga na wanaishi lakini cha ajabu Peter Junior amekuja kuonyesha mipaka ya ekari zaidi ya 200 sasa tunajiuliza huyu mtu hiyo nguvu ya kuwasumbua Wananchi anaipata wapi wakati hapa hana eneo?alihoji mwenyekiti huyo.
Athumani amesema kuwa msimamo wake ni kuwa hukumu inahusu shamba la Peter Maro na sio Wananchi wake 120 hivyo ni vyema Peter Junior aoneshe wawakilishi wa Mahakama ardhi aliyomshinda Peter Maro na sio kucheza na Wananchi wake.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na kwamba kinachotakiwa ni kuhakikisha wanakwenda kuwachagua viongozi wazuri akiwa pamoja na kumchagua Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi ili aweze kuiletea nchi maendeleo zaidi.
Hata hivyo,amesema ili kufikia malengo yao ya kutekeleza aadi ya kumchagua Rais Samia kwa kura nyingi ni vyema kwasasa wakajitokeza kuhakiki katika daftari la kudumu la wapiga kura katika zoezi linaloendelea katika ofisi yao ya Kitongoji ambapo kufanya hivyo itatoa fursa kwenye uchaguzi kufanya maamuzi sahihi.
Katika mkutano huo uliofanyika Mei 20,2025 katika Kitongoji hicho mmoja wa Wananchi hao Elias Kashaga, amesema kuwa anashangazwa kuona Peter Junior amekuwa akiwasumbua na kutaka kupora eneo lao kinyume na utaratibu.
Mwananchi wa Kitongoji cha Kwakibosha Elias Kashaga ambaye ni mhanga wa kubolewa nyumba yake katika eneo hilo akizungumza na Waandishi wa habari.Kashaga amesema kuwa yeye ni mhanga wa eneo hilo ambaye nyumba yake awali ilivunjwa na Peter Junior kwa madai ya kuwa eneo hilo ni lake huku akisema mtu huyo amekuwa akiwatesa sana Wananchi wa eneo hilo.
"Tunaiomba Serikali iingilie kati jambo hili ikiwa pamoja nakumfanyia uchunguzi huyu mtu na ikiwezekana Takukuru,Wizara ya Ulinzi na Vyombo vya vingine vya usalama vimalize jambo hili kwa haraka ili kuzuia hatari inayoweza kutokea hapo baadae,"amesema Kashaga.
Nae Yolanda Mingoi mkazi wa kwa Kibosha amesema kuwa Peter Junior anawafanya Wananchi wakose amani kwa vitisho vyake kwa jamii huku akisema anatumia ujanja na njia zisizo sahihi kutaka kupora ardhi ya Wananchi hao.
Mwananchi wa Kitongoji cha Kwakibosha Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo Yolanda Mingoi akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu adha ya kutaka kubomolewa nyumba zao.Mingoi,ameiomba Serikali ya awamu ya Sita Chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo ili kuwafanya Wananchi hao waishi kwa amani kwakuwa anaamini Peter Junior hana viwanja Wala kipande chochote cha ardhi katika eneo hilo.
Peter Junior akizungumza na Waandishi wa habari kwa njia ya simu amesema kuwa hao watu wanaolalamika walinunua eneo hilo kutoka kwa Ally Mguru kwa mujibu wa dokumenti (documents)zao ambazo walizitoa Mahakamani na hao Wananchi wanaolalamika waliwahi kufungua kesi Mahakama Kuu kesi namba 260 ya Mwaka 2003 na walishindwa.
Junior,amesema yeye haitaji msaada wa kiongozi yeyote na hivyo atabomoa nyumba hizo kwa amri ya Mahakama na kwamba lazima shamba hilo atalichukua kwakuwa ni haki yake.
Post a Comment