ZIKO WAPI MILIONI 50 ZILIZOTOLEWA NA NAIBU WAZIRI MKUU KUJENGA OFISI YA CCM NYANG'HWALE ?
>>Inaelezwa kuwa fedha zilipokelewa na Mbunge wa Jimbo la Nyang'hwale miezi mitatu iliyopita
>> Hadi sasa fedha hazijawekwa kwenye akaunti ya Chama
Na Gustaphu Haule, Geita
KUMEIBUKA utata wa fedha kiasi cha Tsh. Milioni 50 zinazodaiwa kutolewa na Naibu Waziri mkuu , Dotto Biteko kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyang'hwale, mkoani Geita, lakini fedha hizo hazijatumika kwenye ujenzi tangu zitolewe miezi mitatu iliyopita.
Inadaiwa kuwa fedha hizo zilipokelewa na mbunge wa jimbo la Nyang'hwale Hussein Nassoro Amar na kuziweka kwenye akaunti yake binafsi , hadi sasa hajazikabidhi kwenye chama ili kuendeleza ujenzi wa ofisi .
Inaelezwa fedha hizo zilitolewa ili kukamilisha ahadi ya Naibu Waziri Mkuu wakati wa ziara yake Wilaya hiyo mwaka jana ambapo akiwa katika mkutano wa hadhara aliahidi kuchangia Tsh. Mlioni 50 kwa ajili ya kukamilisha jengo la ofisi ya CCM Wilaya.
Kwa mujibu wa baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) wilayani humu majina yao yanahifadhiwa wanasema kwamba, kukwama kwa ujenzi , licha ya fedha kutolewa kumesababishwa na mbunge huyo pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyang'hwale, Adam Mtore.
Inaelezwa kwamba, kiongozi aliyeagiza fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti binafsi ya mbunge ni mwenyekiti wa CCM Adam Mtore ambaye ni mdogo wake na mbunge wa Jimbo hilo.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi katika wilaya hiyo wamekuwa wakijiuliza maswali yasiyopata majibu.
"Shughuli za ujenzi wa jengo la ofisi ya Chama zimesimama kwa madai kwamba hakuna fedha wakati fedha zimetolewa miezi mitatu iliyopita.
"Tunashangaa usiri wa fedha hizo ambao unafanywa na mbunge pamoja na mwenyekiti wa Chama Wilaya ambao ni ndugu ( Kaka na Mdogo wake) wanasema wanaccm.
Mwanachama mwingine anauliza " Je, inawezekana labda mbunge anafanya biashara na fedha za Chama au ameziweka kwenye"Fixed Deposit (Amana ya muda maalum )"ili apate riba kwa manufaa binafsi ? " .
" Kwanini fedha hizo zimekuwa siri ya watu wawili ambao ni ndugu? je kamati ya siasa wanafahamu juu ya fedha hizo ?je CCM mkoa wa Geita wanafahamu kuhusu kufichwa Kwa fedha hizo kwenye akaunti binafsi ya mbunge ? anauliza Mwanachama.
Wilaya ya Nyang'hwale haina jengo jipya la ofisi ya CCM ndani ya mkoa wa Geita licha ya kuwepo Wilaya mpya ambazo tayari zimejenga majengo mazuri yenye hadhi ya Chama cha Mapinduzi huku wanaccm wakihoji aibu hiyo mbunge na Mwenyekiti wa CCM Wilaya hawaioni ?
Wakataa fitina dhidi ya DC
Licha ya mwenyekiti na mbunge kutuhumiwa kutotumia fedha zilizotolewa na Naibu Waziri mkuu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, wanashangaa kuona mwenyekiti na mbunge wakimtuhumu mkuu wa wilaya ya Nyang'hwale, Grace Kingalame kuwa ameshindwa kusimamia ukamilikaji wa jengo.
" Kinachoshangaza zaidi ni kwamba ofisi ya CCM Wilaya hususani mwenyekiti wa CCM Wilaya anamtuhumu mkuu wa Wilaya kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ukamilishaji wa jengo hilo na ameitwa na kamati ya siasa ya Wilaya kwa lengo la kuhojiwa kwanini anahujumu ujenzi wa jengo la ofisi ya CCM Wilaya" anasema Mwanachama.
"Hizi fitina lengo lake ni kumchongea mkuu wa Wilaya kwenye mamlaka yake ya uteuzi ili afukuzwe kazi wakati wenye makosa ni mbunge na mwenyekiti wa CCM Wilaya" anasema Mwanachama mwingine.
CCM Taifa ifanye uchunguzi
Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, anaombwa kufanya uchunguzi kuhusu jambo hilo kwakuwa viongozi hao wawili ni ndugu na hawawezi kuchunguzana na badala yake wanafichiana siri huku wakifanya njama za kutaka mkuu wa Wilaya afukuzwe kazi .
Wanachama wanasisitiza fedha hizo zilizotolewa , ziwe wazi ziweze kutumika kujenga na kukamilisha ofisi ya Chama chao na kwamba wao hawawezi kunyamaza kwani wanachotaka ni kuona CCM wilaya ya Nyang'hwale inaendelea kama wilaya nyingine zilivyoendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale Grace Kingalame amesema yeye hausiki na chochote huku akimtaka mwandishi wa habari atafute wahusika ili apate ufafanuzi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya hiyo , John Isaka amesema kuwa yeye anashughulika na Halmashauri na kwamba akiulizwa swali linalohusu Halmashauri yupo tayari kujibu lakini suala la Chama ni vyema akatafutwa Katibu wa Chama Wilaya au mwenyekiti wa Chama Wilaya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyang'hwale Adam Mtore, alipopigiwa simu Kuulizwa juu ya jambo hilo hakuweza kuweka bayana kama fedha hizo zimetolewa au laa ! lakini alichokisema ni kwamba ni kweli walimuomba kiongozi huyo awasaidie ujenzi wa jengo lao la ofisi ya Chama.
Mtore amesema hajui chochote kuhusu fedha hizo lakini utoaji wa malalamiko katika Chama una utaratibu wake na mara nyingi huanzia ngazi ya chini ya tawi lakini kwakuwa suala hilo linagusa ngazi ya Wilaya wanachama wanaolalamika ilitakiwa wapeleke malalamiko yao kwa Katibu wa Chama Wilaya.
" Na iwapo wasingeridhika wangeenda ngazi ya juu kwa Katibu wa mkoa lakini sio hilo tu,Chama kina vyombo vyake vya kimaadili ambavyo vinaongozwa na Mwenyekiti na Katibu .
" Kama unaona kuna kitu kimeenda kinyume hata huyu Katibu mkuu unakoenda huko ambaye ndiye bosi wetu na mtendaji mkuu wa Chama si atakuuliza hayo mambo taratibu ulizofuata katika kulalamika kwako ?
"Kama Kuna ishu unaona haijaenda sawa ukifika kwa Katibu wa Wilaya hamna ,si utaenda kwa Katibu wa CCM mkoa na ukiona kama nae hajakutendea haki basi utaenda kwa Katibu mkuu wa CCM Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi,"amesema Mtore.
Mtore amesema Naibu Waziri Mkuu hakuahidi kutoa hela lakini aliahidi kusapoti ujenzi ,na ujenzi una kamati kwahiyo aliyekuambia kwamba kuna hela sijui ngapi yeye amejuaje ? alihoji mwenyekiti huyo.
"Mimi Naibu Waziri Mkuu kabla hajawa kwenye hiyo nafasi kipindi hicho ni Waziri wa kawaida ,sasa si unajua wao wanasaidia nchi nzima ,kila sehemu wanaombwa ,kwahiyo amesaidia sehemu nyingi hata Bukombe kwake, Mbogwe ,"amesema Mtore.
"Watu huwa tunaulizana kwamba ukimuona fulani atakusaidia sasa zamu ilikuwa bado lakini mwaka jana alikuja akashuka akaahidi kutusapoti kwenye ujenzi lakini sio kama alitamka kama atatoa fedha " anasema Mtore .
Mbunge wa Jimbo la Nyang'hwale Hussein Nassoro Amar, ameeleza kusitikishwa na malalamiko ya wananchama hao huku akisema jambo hilo halina usiri wowote.
"Mimi kwa maelezo hayo ambayo umenieleza kwanza mimi niseme tu nimefurahi lakini ningeomba unisaidie kidogo, hao wanaosema ni wanachama wa CCM kutoka Nyang'hwale ? . Tuna wanachama 45000 , natamani kujua hao wanachama wametoka Kata gani, wana nafasi gani na hata majina yao "amesema Mbunge Amar.
Amesema kuwa wanachama wanavyosema kuwa mbunge ana Tsh.Milioni 50 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi ni vyema kabla ya kulalamika wangemuuliza Naibu Waziri mkuu wape majibu kama alitoa fedha au la ! kuliko kulalamika bila kuwa na ukweli.
"Kwasababu mimi ndiye niliyeomba atusaidie na sio maramoja na bahati nzuri alipokuja yenye mwenyewe alikumbushia ombi hilo na akakubali kusaidia lakini hakutamka kiwango,"amesema Amar .
"Mwandishi wewe waambie waende kwa Balozi Dkt.Nchimbi atawapokea na kuwasikiliza lakini kabla ya hapo si wangeenda kwanza kwa Naibu Katibu Mkuu Dotto Biteko awathibitishie? lakini najua hilo jambo la kisiasa na watu wanatengeneza siasa lakini ni la muda wa miezi mitatu tu litakwisha "amesema.
Mbunge Amar ameongeza kuwa, kwa sasa hawezi kujieleza sana kwasababu hizo ni tuhuma na zikifika kwa Dkt. Nchimbi ataitwa kwasababu Nchimbi ni bosi wake, na atamuuliza Dkt. Biteko.
" Hakuna mahali Naibu Katibu Mkuu ametamka kutoa Tsh. Milioni 50 nina kumbukumbu sahihi kupitia Nyang'hwale TV kwakuwa siku hiyo walirekodi na wanaweza kurudia kuangalia hayo mazungumzo kwamba wapi alitamka kutoa Tsh. Milioni 50.
"Lakini mbali na hayo mimi kupewa fedha kupitia akaunti yangu kuna uharamu ? , halafu mimi kusema fedha hizi zimepitia kwenye akaunti ya mbunge nadhani sio shida lakini shida inakuja pale wanaposema nina hujumu kwakuwa hii ni kashfa kwangu " amesema mbunge huyo .
Mbunge huyo ameongeza kuwa yeye binafsi amekuwa na mchango mkubwa katika ujenzi wa ofisi hiyo ya Chama kwani alishawahi kutoa mashine zake na magari yake (Tipa) kufanya kazi katika ujenzi huo na kwamba ana hujumu vipi ?" anauliza.
" Malengo yangu ni kujenga ofisi ya Chama nimekuwa nikitafuta wadau kwa kushirikiana na mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale Grace Kingalame ambapo Kingalame amekuwa na mchango mkubwa sana katika usimamizi wa ujenzi wa jengo hilo lakini anashangaa kuambiwa eti tunamuhujumu Kingalame, kivipi? na ili afanyweje ?.
"Mimi sikatai nilipokea hizo fedha, lakini hao wanapozungumza kuwa alitoa kiasi hicho cha fedha , hivi wana uhakika gani kama alitoa yeye? na je, kuna uharamu gani yeye kupewa au kuingiziwa fedha na Naibu Waziri Mkuu? Anahoji mbunge Amar.
Aidha, Amar anasema kuwa fedha hizo zilivyoingia na siku anazipokea alimpa taarifa Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Chama, Mwenezi, kamati ya siasa, na kamati ya ujenzi na yeye mbunge ndiye aliyetafuta fundi na kuwashauri kuwa kuna fundi anaezeka banda lake kwahiyo ni vyema akatumika kwakuwa yupo vizuri katika ujenzi.
" Siku moja nilimwagiza yule fundi kwenda kupima nikasema wakihitaji vifaa waseme kwakuwa mimi navipata vifaa Jijini Dar es Salaam kwa bei nafuu kuliko Mwanza.
"Kwahiyo nikawaambia mtakapokamilisha mniambie maana hela yenu ninayo, na hawajanielekeza niweke kwenye akaunti gani, na kwasababu wananiamini mimi wakati wowote wanajua hela yao ipo salama mikononi mwangu na bahati nzuri nilisharipoti kwao na zaidi mimi sipo kwenye kamati ya ujenzi " anasema mbunge.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa baada ya Naibu Waziri Mkuu kumuambia fedha hizo zipo tayari zitaingizwa kwenye akaunti ndipo akachukua jukumu la kuripoti kwa viongozi wote na wanajua.
"Lakini mimi ndiye niliyeomba , mimi ndiye niliyezungumza nae, mimi najua tumetoka wapi na Biteko na hata katika mkutano Biteko aliwaambia tulikotoka na akasema huyu ndiye mwenyekiti wetu wa wabunge wa mkoa wa Geita na ndio maana hela ilipokuwa tayari akanipa kinoti akanielekeza niende wapi kuchukua ,"amesema.
"Hela ipo mikono salama na hata Mei 03, 2025 niliongea na mkuu wa Wilaya kumweleza juu ya fedha zao kwamba zinatakiwa kufanya kazi iliyokusudiwa kwakuwa mimi sitaki kukaa na huo mzigo ,nipeni akaunti niwahamishie.
" Lakini Kingalame amesema atakaa na kamati yake ya ujenzi na akasema wakati huu niendelee kukaa nazo na wakihitaji kununua vifaa watanijulisha ili nitoe hizo fedha",ameongeza Amar.
Amesema kuwa jambo lolote la kufichiana siri kati yake na Mwenyekiti wa CCM Wilaya halipo ndio maana baada ya kupata hela hizo alizungumza moja kwa moja ndani ya kikao cha kamati ya Siasa, kamati ya ujenzi na kuwapa njia sahihi za kupunguza gharama kwakuwa jengo hilo ni kubwa.
Amesema yeye na mkuu wa Wilaya wapo vizuri na wanashirikiana vizuri na Nyang'hwale imetulia na ipo salama kwakuwa wanafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi zote, idara zote ,ofisi ya mkurugenzi, ofisi ya DC, Chama na wananchama wake pamoja na wananchi kiujumla.
Post a Comment