SHAIRI: NENDA NA BARAKA ZAKO
AMEIGA dunia, huku wengi wamwimbia,
Nyimbo za kumlilia, jinsi alijiishia,
Kama hukumsikia, pole kwako nakwambia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda baraka zako.
Wengi ni kumsikia, ndiko tunasimulia,
Jinsi alituingia, kazi akijifanyia,
Moyoni akibakia, sauti kijirudia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Kila achoshikilia, ukimsikilizia,
Lazima kufurahia, jinsi alikijulia,
Mungu alimjalia, kuibariki dunia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Hasa kututangazia, hapa na kwenye dunia,
Kote tulifurahia, hata mfuatilia,
Yake yalituingia, na kutuambukizia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Macharanga kumbukia, nani aliyajulia,
Au kufuatilia, toka pande za dunia,
Nkwanga lipoingia, wengi tuliyadandia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Kizuri watuambia, wahenga nakumbukia,
Debe si kujipigia, mabango kutangazia,
Wenyewe wanakijia, wazidi kifaidia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Habari lizijulia, kama kikutangazia,
Michezo limsikia, alivyotuchambulia,
Nini achoshikilia, ambacho tulisinzia?
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Watangazaji sikia, nyote mnomlilia,
Kilio cha Tanzania, kile kimetufikia,
Vile twamkumbukia, toka alikoanzia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Hata alikoishia, nako tulifurahia,
Sauti tukisikia, ya Rais kutwambia,
Yote ilikumbushia, jinsi tulimzimia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Sifa nyingi twasikia, wengi wanammwagia,
Jinsi aliwaingia, mengi wakijifunzia,
Kwa wale wanabakia, ni somo kuigizia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Pole za kuwafikia, wote wale wanalia,
Kwa yaliyotufikia, ni wengi tunaolia,
Hii yatukumbushia, siyo ya kwetu dunia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Pole sana familia, haya yalowafikia,
Mungu kumkimbilia, ndiye faraja sikia,
Serikali pole pia, mtumishi kaishia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Kote alikopitia, kazi akitufanyia,
Majonzi yalowajia, nasi yanatuingia,
Wapweke tumebakia, twavyojisikitia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Mungu alotupatia, kuibariki dunia,
Ndiye kajichukulia, jinsi alivyoishia,
Sisi yote twamwachia, kwa majonzi twatulia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Sisi tunaobakia, kifo hakijatujia,
Hili lakufikiria, maisha kuangalia,
Watu wanafurahia, au ndiyo wanalia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Vema watu wafanyia, mema ya kukulilia,
Siyo ukitangulia, ahueni wasikia,
Hapa tunaangalia, mwenzetu wamlilia,
Charles Hilary Nkwanga, nenda na baraka zako.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment