HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU KAGERA YAOKOA MILIONI 50.3 MRADI WA UJENZI HOSPITALI YA MISSENYI

Alodia Dominick,  Bukoba 

TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera imedhibiti upotevu wa Tsh. Milioni 50.3 katika mradi wa ujenzi hospitali ya wilaya Missenyi.

Pia imerudisha fedha za wananchi tisa Tsh. Milioni 2.3 wilaya ya Muleba  waliokuwa wamedhurumiwa fedha kupitia mradi wa wakala wa umeme vijijini (REA) uliokuwa unatekelezwa na kampuni ya Nakuroi Investinent ltd.

Kwa mujibu wa Kaimu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera Hajinas Onesphory akitoa taarifa ya miezi mitatu, Januari -Machi, 2025 kwa waandishi wa habari ameeleza kuwa, taasisi hiyo katika ufuatiliaji ilibaini kutokuwepo na kutotumika kwa vigae (tiles) zenye thamani ya Tsh. Milioni 50.3 katika hospitali ya wilaya ya Missenyi.

     Kaimu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera Hajinas Onesphory akitoa taarifa ya miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu kwa  waandishi wa habari.

Amesema vigae hivyo havikuwasilishwa kwenye mradi huku nyaraka zote za manunuzi na mapokezi zikionyesha kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa na kupokelewa kwenye eneo la mradi.

Ameeleza kuwa baada ya TAKUKURU kubaini hilo ilifuatilia kwa kina kwa kumshirikisha mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi ili kuhakikisha vigae hivyo vinapatikana.

"Hadi sasa mzabuni awewasilisha vigae vyote kwenye eneo la mradi na vimetumika kama ilivyokusudiwa na hatua dhidi ya watuhumiwa zitachukuliwa pindi uchunguzi utakapokamilika" amesema Onesphory 

Wakati huo huo, wananchi tisa wa kijiji cha Bulembo kata ya Ibuga wilaya ya Muleba waliokuwa wamedhurumiwa kwa kuchangishwa fedha Tsh.Milioni 2.3 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme kupitia mradi wa Wakala wa barabara vijijini REA uliokuwa unatekelezwa na Kampuni ya Nakuroi Investinent ltd.

         Wananchi tisa katika wilaya ya Muleba waliokuwa wamedhurumiwa fedha zao na leo wamerudishiwa fedha zao na TAKUKURU.

Amesema kijiji hicho hakikuwa katika mpango wa kufikishiwa umeme kwa wakati huo hivyo mafundi hao waliwalaghai wananchi watoe fedha hizo ili wapelekewe umeme huku wakijua wazi kuwa jambo hilo haliwezekani.

"Baada ya TAKUKURU kupata taarifa hizo uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa wawili walifikishwa mahakamani kwa makosa ya Rushwa na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu" amesema Onesphory 

Ameeleza kuwa, mahakama ya wilaya ya Muleba baada ya kusikiliza shauri hilo mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Daniel Nyamkyelya iliwatia hatiani washtakiwa wawili ambao ni Patrick Muchunguzi na Revocatus Masanja kwa makosa ya udanganyifu chini ya kifungu namba 15 cha kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na adhabu nyingine.

Hakimu aliamuru fedha zote zilizochukuliwa na watuhumiwa Tsh. Milioni 2.3 zirudishwe na kurejeshwa kwa wananchi husika kupitia ofisi ya Takukuru na fedha hizo zimerejeshwa leo kwa wananchi hao tisa.

Mmoja wa wananchi waliorejeshewa fedha yao Akwilina Philimon ameishukuru taasisi hiyo kwa jitihada zao walizofanya na kurudishiwa fedha yao ambayo hawakuwa na matarajio ya kuipata.

        Kaimu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera Hajinas Onesphory akitoa fedha kwa mmoja wa wananchi waliokuwa wamedhurumiwa wilaya ya Muleba Alodia Modest.

      Anayepokea fedha ni Joselina Felix kiasi cha sh.200,000 mmoja wa wananchi waliokuwa wamedhurumiwa fedha.

No comments