SHAIRI : WAGUNDUZI, WAVUMBUZI

NI Bonde la Siliconi, maarufu Marekani,
Si kwa mambo yale duni, ni yale ya kileleni,
Sasa kote duniani, wana zao Siliconi,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Waliona Marekani, kwa kufikiri kichwani,
Lije Bonde Siliconi, kuwatoa msambweni,
Teknoloji za chini, zote wazipige chini,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Bidhaa zilizo duni, fedheha mitandaoni,
Zote zaishia chini, wakiushika mpini,
Wanafikiri kichwani, na vitu kuja mwilini,
Wagunduzi wavumbizi, wengi huanza bondeni.
Kufikia kileleni, na ugunduzi makini,
Wakubwa tia mifukoni, vijana wende kazini,
Hata wawe vitandani, akili ziwe angani,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Hawatulii mezani, na soga za mdomoni,
Wanaenda vitabuni, kujua vitu kindani,
Kisha huko viwandani, hufanya vitu makini,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Hizi simu mkononi, kurusha pesa hewani,
Kisha waenda dukani, pata fedha mfukoni,
Ni Bonde la Siliconi, watikisa duniani,
Wagunduzi, wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Waharibifu makini, waja na vitu makini,
Waweza anguka chini, lakini wajiamini,
Wazidi kuna kichwani, kuleta vitu mwilini,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Afrika hatuko chini, mabonde ya Siliconi,
Tunayo mengi madini, bidhaa za viwandani,
Hata malipo hewani, kwa kweli hatuko chini,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Serikali duniani, na hata hapa nchini,
Ni bora zikae chini, kuzijenga Siliconi,
Vijana wengi nchini, nao waende kazini,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Tanzania makampuni, nanyi ingia kazini,
Anzisheni Siliconi, kwa mapinduzi nchini,
Bila miiba njiani, tutafika kileleni,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Vipaji hivi leeni, nasi tuwe kileleni,
Msilete upinzani, vyote vifie gizani,
Kama Bonde Siliconi tukatambe duniani,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Tafuta vichwa nchini, mijini na vijijini,
Vitumike na kubuni, bidhaa za kileleni,
Tukatambe duniani, kama Bonde Siliconi,
Wagunduzi wavumbuzi, wengi huanza bondeni.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment