HEADER AD

HEADER AD

TAWEN YAHAMASISHA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI KUFUNGA MITAMBO WA JIKO LA GESI


Na Gustaphu Haule, Pwani

MTANDAO wa kuwawezesha wanawake  Tanzania (TAWEN) umeanzisha programu maalum ya kuhamasisha shule za msingi na sekondari kufunga mtambo wa jiko la gesi la kupikia ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan juu ya matumizi ya Nishati Safi.

TAWEN  imeanzisha kampeni hiyo  katika shule ya msingi Ruvu JKT iliyopo Kibaha Vijijini mkoani Pwani ambapo mpaka sasa tayari shule hiyo imejenga mtambo wa jiko la gesi la kupikia kupitia kampuni ya gesi ya O- Gas huku malengo yake ni kufika Tanzania nzima.

Mkurugenzi mtendaji wa TAWEN  Florence Masunga , amesema kuwa anatambua umuhimu wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia na kwakutambua hilo wameona ni vyema wakamuunga mkono Rais Samia kwa ajili ya kutimiza malengo yake.




Masunga amesema kuwa programu hiyo iliyoanzia katika shule ya msingi Ruvu JKT itakuwa kampeni endelevu kote nchini ambapo malengo yake ni kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Amesema katika kufanikisha malengo ya utekelezaji wa kampeni hiyo , TAWEN itakuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha kama vile NMB Benki,UTT - AMIS ,O- Gas,wadau wengine ,Wananchi na Serikali kupitia Halmashauri zake.

" Tunamshukuru Rais Samia kwa kuanzisha jambo hili muhimu la matumizi ya Nishati Safi na sisi kama Taweni tumeona ni vyema tukamuunga mkono mwanamke mwenzetu ili kuhakikisha elimu hii ya matumizi ya Nishati Safi inafika kote nchini Kwa vitendo ,"amesema Masunga

Masunga amesema matarajio ya TAWEN ni kuona kila shule au taasisi zenye watu kuanzia 100 wanatumia Nishati safi ya kupikia kwa kufunga mtambo wa jiko la gesi huku akisema lengo ni kuhakikisha ifikapo 2034 matumizi ya nshati safi yawe yamefika kila kona ya Tanzania.

     Afisa masoko wa kampuni ya O-Gas Ally Rajabu(kushoto) akimkabidhi makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibaha Vijijini Halima Jongo mtambo wa jiko la Nishati Safi ya kupikia.

Kuhusu mtambo wa jiko la gesi uliofungwa shule ya msingi Ruvu JKT amesema kuwa mtambo huo awali umefungwa kwa mali  kauli na kampuni ya O-Gas huko utaratibu wa malipo ukifanyika taratibu kupitia harambee maalum.

Masunga amesema kuwa harambee ya kuchangia malipo ya kufunga mtambo wa Nishati safi ya kupikia shuleni hapo imefanyika Mei 24,2025 ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza kuchangia wakiwemo NMB Benki waliochangia kiasi cha Sh .milioni tano.

Wengine waliochangia katika harambee hiyo ni UTT- AMIS wakitoa T sh. Milioni moja, Halmashauri ya Wilaya Kibaha Vijijini ikitoka Tsh.Milioni moja, TAWEN ikitoa TSh .laki tano,O-Gas ikitoka laki tano pamoja na nguvu za Wananchi ambapo jumla ya Tah.milioni 8,164 ,450 zilipatikana.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano ya mtambo huo Mwalimu wa shule hiyo Nuru Mwamfumu, amesema kuwa mradi huo ulianza kujengwa Aprili 20,2025 kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo mapato ya Halmashauri, walimu na michango kutoka kwa wazazi.

     Mwalimu wa Shule ya Msingi Ruvu JKT iliyopo Kibaha Vijijini Nuru Mwamfumu akitoa taarifa ya ujenzi wa mtambo wa jiko la Nishati Safi.

Amesema kuwa baada ya kukamilika ujenzi wa jengo la jiko hilo ,Tawten kwa kushirikiana na O-Gas walifanikisha kufunga mtambo wa jiko la Nishati safi ya kupikia ambao ni salama kwa mazingira ya Shule hiyo.

Ametaja faida za kufunga Nishati Safi ya kupikia Shuleni hapo kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za kupika chakula cha wanafunzi,uokoa muda,kupunguza magonjwa ya mapafu na saratani na kupunguza hewa ukaa katika uso wa dunia inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi .

Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini Evelyn Ngwira, amesema jambo la matumizi ya  Nishati Safi ya kupikia ni muhimu na utekelezaji huo ni agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ngwira, amesema Shule ya Msingi Ruvu JKT ni mfano kwani anategemea shule nyingine zinakwenda kutekeleza agizo hilo na kwamba kila Shule yenye wanafunzi zaidi ya 100 mpango huo utafanyika kupitia wadau mbalimbali hususani O- Gas.

Afisa masoko wa kampuni ya O-Gas Ally Rajabu amesema kuwa wamefunga mtambo wa Nishati Safi ya kupikia Shuleni hapo kwa ajili ya kuiunga mkono Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ambayo inataka ifikapo 2034 asilimia 80 ya taasisi za Serikali na binafsi ziwe zinatumia Nishati Safi.

      Afisa masoko wa kampuni ya O-Gas Ally Rajabu akionyesha sehemu ya mtambo wa Nishati Safi ya kupikia uliofungwa katika Shule ya Msingi Ruvu JKT iliyopo Kibaha Vijijini Mkoani Pwani.

Rajabu amesema kuwa kampuni ya O-Gas ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tawen kwa ajili ya kuhakikisha Shule zote nchini pamoja na taasisi ambazo zinapika chakula kuanzia watu 100 zinahamasishwa kufunga mtambo huo.

Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini Halima Jongo,ameipongeza taasisi ya Tawen kwa kuona umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi na kufunga mtambo wa jiko la gesi Shuleni hapo.

      Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini Mkoani Pwani Halima Jongo katika kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi Ruvu JKT.


Ameiomba taasisi ya TAWEN pamoja na washirika wake kuendelea na programu hiyo muhimu na kuhamasisha Shuleni nyingine kutumia Nishati Safi ya kupikia ili kuweza kufikia malengo ya Rais Dkt.Samia Suluhu.

      Washiriki wa harambee ya kuchangia malipo ya mtambo wa Nishati Safi ya kupikia katika Shule ya Msingi Ruvu JKT iliyopo Kibaha Vijijini Mkoani Pwani

No comments