UKOSEFU WA WALINZI USIKU KATIKA ZAHANATI WADHOOFISHA HUDUMA ZA AFYA
Na Samwel Mwanga, Maswa
CHAMA cha Wauguzi mkoa wa Simiyu kimeeleza kuwa ukosefu wa walinzi wa usiku katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya zahanati ni mojawapo chanzo kikubwa cha wananchi kukosa huduma za afya za dharura nyakati za usiku.
Akisoma risala ya wauguzi hao Mei 23,2025 katika maadhimisho ya siku ya Wauguzi yaliyofanyika kimkoa katika wilaya ya Maswa, Katibu wa Chama cha Wauguzi mkoa wa Simiyu, Epafra Charles, amesema kuwa zahanati nyingi zinakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uwezo wa kuajiri walinzi.
Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Simiyu, Epafra Charles akisoma risala ya wauguzi wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi ambayo ilifanyika katika wilaya ya Maswa mkoani humo.Amesema kuwa hali hii inawalazimu watoa huduma kubaki majumbani mwao nyakati za usiku na kushindwa kuhudumia wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
“Ulinzi sehemu za kazi ni jambo la muhimu sana kuna baadhi ya zahanati zinakosa uwezo wa kuajiri walinzi na jukumu hili limebaki kuwa la wafawidhi wa zahanati bila halmashauri ya wilaya na serikali ya kijiji kuhusika moja kwa moja,”
“Mapato ya zahanati hizo hayatoshelezi na hasa ukizingatia huduma za wateja katika ngazi ya zahanati wengi wao ni watoto,wajawazito na wazee ambao huduma zao hazilipiwi,”amesema.
Amesema kuwa Chama cha Wauguzi kinatoa wito kwa halmashauri za vijiji na mamlaka husika kushirikiana kwa karibu na vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya zahanati ili kuhakikisha mazingira salama kwa watoa huduma na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi hasa nyakati za dharura.
Baadhi ya wauguzi wa afya wakila kiapo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wauguzi yaliyofanyika wilayani Maswa.“Hali hii ni ya kusikitisha, kwani afya na maisha ya wananchi wako hatarini kwa sababu tu ya kukosekana kwa ulinzi,watoa huduma hawawezi kujitokeza nyakati za usiku bila uhakika wa usalama wao,” amesema.
Amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa wauguzi na wakunga wanachukua asilimia 60 ya wataalam wote wa afya nchini na asilimia 80 ya kazi zote hufanywa na wenyewe hivyo ni muhimu sana mazingira yao ya kufanya kazi hasa nyakati za usiku yanatakiwa kuwa ya usalama zaidi.
“Sisi ndiyo tuko karibu zaidi na wagonjwa pamoja na jamii katika maeneo yetu hivyo mazingira yetu wakati wa ufanyaji wa kazi za nyakati za usiku ambazo huwa ni dharula hasa kwenye zahanati zetu tunahitaji usalama wa kutosha,”amesema.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amewaagiza wakuu wote wa wilaya katika mkoa huo kuhakikisha zahanati na vituo vya afya ambavyo havina walinzi wanakuwepo.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi (kushoto) akimkabidhi tuzo mmoja wa Wauguzi (kulia)ambaye ni miongoni mwa wafanyakazi hodari.“Wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Simiyu hakikisheni katika maeneo yenu ambapo kuna zahanati na vituo vya afya vyote vinakuwa na walinzi ili huduma za afya ziweze kutolewa nyakati za usiku,”amesema.
Kihongosi pia amewakumbusha wauguzi hao kufanya kazi kwa kufuata maadili ya kazi zao huku akisisitiza kuwepo na umoja,upendo na mshikamano kwa watumishi wa kada ya afya katika mkoa huo.
“Tunawathamini kwa kazi mnazozifanya kutuhudumia hivyo fanyeni kazi kwa kufuata maadili ya kazi yenu na msitengenezeane ajali katika maeneo ya kazi kwa lengo la kumharibia mwingine cha msingi dumisheni umoja,upendo na mshikamano,”amesema.
Katika maadhimisho ya siku ya Wauguzi mwaka huu yalibeba kauli mbiu isemayo”Uuguzi Nguvu ya mabadiliko duniani”.
Post a Comment