UWEKEZAJI KILIMO
KWENYE uchumi kilimo, mchango mkubwa sana,
Ajira ni nyingi humo, wazee hata vijana,
Chakula ni humo humo, tuna uhakika nguna,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Sitini hadi sabini, ni asilimia ona,
Watu walio kazini, wanalima na kuvuna,
Watapakaa nchini, kila pande twawaona,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Ni kwa asili mia, twala tunachokivuna,
Na nje ya Tanzania, nako tunauziana,
Kwenye pato Tanzania, kinachangia kw asana,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Kwenye pato la taifa, kilimo muhimu sana,
Asilimia za dhifa, ishinatisa twaona,
Kinazibaziba ufa, mapungufu tukiona,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Tembelea viwandani, kilimo muhimu sana,
Malighafi viwandani, huko zatumika sana,
Hizo zazidi sitini, asilimia twaona,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Ni bidhaa za kilimo, ndizo ziko mbele sana,
Kwa mauzo nje zimo, asili ni nyingi sana,
Themanina tano humo, nje tunauza sana,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Hapa kwetu Tanzania, wengi wetu twafanana,
Kilimo twakitumia, maisha yetu kufana,
Mafanikio sikia, kilimo tunakiona,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Kama wataka kulima, bado nchi kubwa sana,
Wala usishike tama, endelea kupambana,
Ukitaka kusimama, kilimo muhimu sana,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Mazao ya biashara, tunalima mengi sana,
Visiwani hata bara, yanaleta pesa sana,
Tukizidisha ubora, tutaongeza kuvuna,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Yapo pia ya chakula, twajitosheleza sana,
Ugali wali chakula, hivyo tunapenda sana,
Mifugo pia chakula, nayo tunafuga sana,
Uwekezaji kilimo, ukombozi wa kudumu.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment