USHINDI WA PROFESA JANABI NI WETU

HILI la Janabi letu, kwani huyu bingwa wetu,
Hapa mtumishi wetu, hadi Afrika ni yetu,
Kuchaguliwa mwenzetu, heko Serikali yetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Toka Muhimbili yetu, kwenda WHO shirika letu,
Hiyo hadhi kubwa kwetu, kwa Afya ya Bara letu,
Huyu mbobezi wetu, masuala Afya yetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Kampeni za nchi yetu, kinara Rais wetu,
Zainua watu wetu, kimataifa ni kwetu,
Tunazo hesabu zetu, hawa watalamu wetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Juzi Ndugulile wetu, alikwaa kiti chetu, akawa siyo mwenzetu, mauti ikaja kwetu,
Twaonesha tuna watu, kimataifa ni kwetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Juzi Dokta Ntuli wetu, kanyosha bendera yetu,
Naye huyu ni mwanetu, huko mwakilishi wetu,
Zote ni kampeni zetu, tena ushindani wetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Kimataifa wenzetu, washika nyadhifa zetu,
Kwa hiyo wajibu wetu, tuwaombee wenzetu,
Huko wakafanye vitu, ustawi Bara letu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Hongera Janabi wetu, kuwa Mkurugenzi wetu,
Kanda WHO Afrika yetu, ziwe njema afya zetu,
Uliyoyafanya kwetu, kazidishe kwa wenzetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Watafurahia watu, kwa kutosikika kwetu,
Maonyo mazuri kwetu, kuhusu ulaji wetu,
Afrika yako yetu, kasema na sote watu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Ingawa hubaki kwetu, tunabaki roho kwatu,
Elimu ya kwako kwetu, hiyo inabaki kuntu,
Tutajali afya zetu, kwa maisha mema yetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Kulakula hovyo kwetu, hizi nyamachoma zetu,
Na hivi vinywaji vyetu, athari kwa mili yetu,
Tumepunguza mwakwetu, tuko gado afya zetu,
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Heri kwako bingwa wetu, majukumu yako yetu,
Kwako tutapata kitu, na Waafrika wenzetu,
Zidi kuwajibika tu, akutunze Mungu wetu
Profesa Janabi wetu, ushindi wake ni wetu.
Mtuzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment