DUNIA YETU DUARA

KAMA ndege yuko hai, yeye ndiye hula mchwa,
Akipoteza uhai, yeye huliwa na mchwa,
Ishi bila kujidai, ni mchana kutakuchwa,
Dunia yetu duara, ishi kwa unyenyekevu.
Unaishi uko hai, kwenye kiota wafichwa,
Unakula mapapai, wengi chini wameachwa,
Hata kama una tai, wala usivimbe kichwa,
Dunia yetu duara, ishi kwa unyenyekevu.
Wahenga hawachakai, busara yao twavikwa,
Aliye juu hakai, juu huko atachokwa,
Chini atakunywa chai, bila mkate kuokwa,
Dunia yetu duara, ishi kwa unyenyekevu.
Ni bingwa hatukatai, huku chini tumeachwa,
Milele huko hukai, nawe siku utaachwa,
Sawa na mchaichai, kinyauka utaachwa,
Dunia yetu duara, ishi kwa unyenyekevu.
Kweli wewe uko hai, unakula kama mchwa,
Kwa sasa hauchakai, jinsi umevimba kichwa,
Jua chini kwakudai, utambue utashushwa,
Dunia yetu duara, ishi kwa unyenyekevu.
Kama hujidaidai, na wala huvimbi kichwa,
Hata uvuliwe tai, na watu huwezi achwa,
Utakuwa huchakai, vile huwezi kukachwa,
Dunia yetu duara, ishi kwa unyenyekevu.
Wewe ndege uko hai, sasa zidi kula mchwa,
Ukiondoka uhai, takuja liwa na mchwa,
Kwa vile wazua mbwai, chini huko utafichwa,
Dunia yetu duara, ishi kwa unyenyekevu.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment