HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAVUNJA BARAZA LA MADIWANI
>>Mapato yaongezeka kutoka Bilioni 3 .8 mwaka 2020 hadi Bilioni 20 mwaka 2025
Na Gustaphu Haule , Pwani
HALMASHAURI ya Mji Kibaha mkoani Pwani imevunja rasmi Baraza lake la Madiwani huku kukiwa na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana ndani ya kipindi cha mwaka 2020/2025.
Baraza hilo limevunjwa Juni 17, 2025 na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Katibu wa Jumuiya wa Wazazi wa Wilaya ya Kibaha Mjini Latifa Semwanza,Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon pamoja na wakuu wa idara wa Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba akizungumza katika kikao hicho amesema kuwa Kibaha Mjini imepata mafanikio makubwa yaliyopelekea Kibaha kuwa na Maendeleo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Musa Ndomba katika kikao maalum cha kuvunja rasmi Baraza la Madiwani Juni 17,2025.
Ndomba amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano tangu 2020 hadi 2025 Kibaha mjini cha madiwani hao wamefanikiwa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani kutoka Tsh.Bilioni 3.8 ya mwaka 2020 mpaka kufikia bilioni 14 ya mwaka 2024.
Ameongeza kuwa,katika kipindi cha mwaka 2024 /2025 mapato hayo yameongezeka zaidi ambapo mpaka sasa tayari wamekusanya kiasi cha Tsh.Bilioni 20 sawa na asilimia 200.
Ndomba amesema kuwa kupitia mapato hayo Halmashauri kupitia Baraza la Madiwani wamefanikiwa kujenga shule za msingi 11 ambapo kati ya hizo Shule tatu ni za mchepuo wa Kiingereza.
Mbali na shule za msingi lakini pia wamejenga shule za Sekondari tisa na kukarabati shule kongwe 17 kwa mapato ya ndani huku vituo vya afya viwili kikiwemo kituo cha Pangani na Kongowe huku Zahanati mpya tisa.
Sambamba na hayo lakini pia baraza limefanikiwa kukamilisha ujenzi wa jengo la Halmashauri, kukamilisha mradi wa ujenzi wa soko la Kisasa la Kibaha Shopping Mall ,machinjio ya Kisasa pamoja na maegesho ya magari.
Amesema kuhusu miundombinu ya barabara Ndomba amesema Kibaha mjini imefanikiwa kuongeza mtandao wa barabara za lami ,kuimarika kwa miundombinu ya umeme, maji na huduma nyingine za kijamii.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya madiwani, mkurugenzi wa Mji Kibaha Dkt.Roger's Shemwelekwa, Wakuu wa idara pamoja na watendaji mbalimbali.
Amempongeza mkurugenzi huyo kwa kazi nzuri aliyoifanya huku akimuomba kuendelea kuchapakazi kwa maslahi ya Wananchi wa Kibaha Mjini.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt . Shemwelekwa amesema kukamilika kwa miradi hiyo pia kumetokana na mchango mkubwa wa Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akitoa pesa nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa katika kikao cha kuvunja Baraza la Madiwani Leo Juni 17,2025.
"Kipekee nawashukuru madiwani wote, Mbunge na Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano mkubwa uliokuwepo lakini shukrani hizi ziende kwa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi ya kutekeleza miradi ya maendeleo," amesema Shemwelekwa
Dkt.Shemwelekwa amewaomba Madiwani hao kwenda kuyasemea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chao kwa wananchi ili kusudi waweze kupata nafasi ya kurudi katika uchaguzi mkuu.
"Mimi nimeteuliwa na Rais Dkt.Samia na hapa nilipo nasimama na Dkt.Samia kwakuwa yeye ndiye aliyenifanya leo niwe mkurugenzi hapa Kibaha Mjini, hivyo lazima tuyaseme vizuri yale yaliyofanywa na Rais,"amesema Shemwelekwa
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amesema madiwani na Mbunge Koka wamefanyakazi njema hivyo wasijiwekee mipaka kwakuwa anaamini wote wanaweza kurudi katika kipindi kijacho.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon akizungumza katika Kikao maalum cha kuvunja rasmi Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Kibaha Juni 17,2025.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Silvestry Koka ameungana na madiwani ,wakuu wa idara na watendaji wa Halmashauri hiyo kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika ndani ya miaka mitano.
Koka amewaomba watendaji na Wakuu wa idara kuendelea kushirikiana kikamilifu ili kusudi waweze kufanya kazi za kuhakikisha Halmashauri inaendelea Kusimama katika suala nzima la maendeleo .
Hata hivyo Koka amempongeza mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kuleta mabadiliko makubwa ya ukusanyaji wa mapato na hata namna ya kufanyakazi.
Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakiwa na mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt.Rogers Shemwelekwa mara baada ya kuvunja baraza hilo Juni 17,2025.
Post a Comment