NI WATU WA MITANDAO
SASA maisha ya kwetu, umimi u hatamuni,
Siku hizi simu zetu, hasa zile mkononi,
Ndiyo ufahamu wetu, umeingia gizani,
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Kazi kuchatichati tu, umbea wa duniani,
Yuko wapi babu wetu, atupe mema zamani?
Yajae vichwani mwetu, hazina ya uzeeni?
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Hii mitandao yetu, si ya jamii nchini,
Hao maadui zetu, kuua yetu zamani,
Inakula muda wetu, tunahama duniani,
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Kukumbatiana kwetu, tukikutana njiani,
Kutembeleana kwetu, kuwa hali ya ugeni,
Jinsi tulifanya kwetu, sasa mambo ya zamani,
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Siyo kwa kutaka kitu, salamu zile nyumbani,
Au kumsema mtu, umbea wa duniani,
Likuwa mila yetu tu, imeshatupwa shimoni,
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Leo miaka ya kwetu, twakutana misibani,
Tunalazimishana tu, kukutana harusini,
Hayo ndiyo mambo yetu, tuliopo duniani,
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Zamani aumwe mtu, twamiminika nyumbani,
Nasi kwa faraja yetu, anapata ahueni,
Na tena siyo sisi tu, huja pia majirani,
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Mtu hamjali mtu, nchini na ugenini,
Sana sana kama mtu, ni kwa simu mdomoni,
Mwenyewe ni ubize tu, auenzi maishani,
Ni watu wa mitandao, ya kale siyo dhahabu.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment