MAHAKAMA : MANENO YA KASHFA YALIYOTOLEWA NA MBUNGE WAITARA DHIDI YA MASWI HAYAKUWA NA UKWELI WOWOTE
>>Mahakama Kuu Kanda ya Musoma yamtaka Waitara, Mwandishi wa habari kumlipa Eliakim Maswi Bilioni 6
>> Mahakama yamzuia Mbunge Waitara , Mwandishi wa habari kurusha kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vyovyote vya habari kuhusu Maswi
>> Maswi aliwaomba Waitara na wenzake waombe msamaha lakini walikataa
Na Dinna Maningo, Musoma
MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Musoma imesema kuwa baada ya uchambuzi, imejiridhisha kuwa maneno ya kashfa yaliyotolea na mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara yalilenga kumchafua Eliakim Chacha Maswi.
Jaji wa mahakama hiyo Mh. Marlin Komba, akitoa hukumu Juni, 16, 2025 kwa wadaiwa watatu ambao ni mbunge Mwita Waitara , Chombo cha habari cha Mara TV, Mwandishi wa Habari Karoli Jacob, amesema mahakama imetoa zuia kuwataka wadaiwa hao kuacha kurusha kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vyovyote vya habari kuhusu Eliakim Maswi.
Alisema mahakama imetoa funzo kwamba mdai ambaye ni Elikim Maswi alipwe fidia ya adhabu Tsh. Bilioni 1 , kwa kile ambacho wadaiwa wamekifanya ambacho hakikuwa na ukweli wowote .
Mahakama hiyo imetamka mdai alipwe fidia ya jumla ya Tsh.Bilioni 5, kwa madhara ambayo wamesababisha. Mahakama imetamka wadaiwa wote waombe msamaha kwa njia ile ile waliyotumia kumdhuru mdai, kurusha maneno ya kashfa hadharani na kwenye mitandao ya kijamii.
" Mahakama hii inatamka wadaiwa wote walipe gharama kwa shauri hili imeamliwa hivyo " alisema Jaji Marlin
Jaji Marlin alisema mlalamikaji Eliakim Maswi ambaye ni katibu mkuu wizara ya katiba na sheria alifungua kesi ya madai namba, 23 ya mwaka 2023 ambapo mdai aliwashitaki wadaiwa hao watatu .
" Malalamiko ya mleta maombi yanasema wadaiwa walitamka mambo yasiyofaa dhidi yake kwamba mbunge Mwita Waitara amemdhalilisha kwamba Eliakim Maswi ni mla rushwa , mtu ambaye anatumia nafasi yake ambaye ni mtumishi wa umma akiwa mtendaji mkuu wa mamlaka ya kudhibiti ununuzi wa umma (PPRA).
" Mdai alisema mambo hayo sio ya kweli na siyo sahihi na hivyo yanalenga kumchafua yeye na kushusha hadhi yake katika jamii na hivyo kuwashtaki wadaiwa watatu ambao ni mbunge Mwita Waitara, Mara TV, na mwandishi wa Habari, Karoli Jacob, akiwalalamikia kwamba wamefanya udhalilishaji kwake bila sababu za msingi.
Jaji huyo wa mahakama alisema kwamba mlalamikaji Eliakim Maswi tarehe 9, 8, 2023 , mlalamikiwa mbunge Waitara aliendesha mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mtana, Kata ya Manga uliowashirikisha watu wengi ambapo inasemekana katika mkutano huo mdaiwa alitamka maneno ambayo hayakuwa sawa na yalishusha hadhi ya mdai.
" Mdai ni mtumishi wa umma ambaye wakati anakutwa na madhara hayo alikuwa ni mtendaji mkuu PPRA . Maneno hayo ya udhalilishaji yalionekana kutamkwa na mdaiwa wa kwanza kwa jina la Mwita Mwikwabe Waitara , huyu ni mbunge wa jimbo la Tarime vijijini .
" Kulingana na nyaraka ambazo nimezipokea mbunge huyo mnamo tarehe 10,8/2023 alishirikiana na wadaiwa namba 2 na namba 3 kwa pamoja waliandaa , walichakata, walichapisha taarifa ya kikao kilichoketi tarehe 9/8/2023 ambacho kilikuwa kina mshambulia kwa madhara mdai.
" Walipandisha habari katika vyombo vya habari ikiwemo YouTube Channel iliyorushwa Mara TV na mdaiwa namba 3 inasemekana tarehe 13 /8/2023 siku chache baada ya kurushwa machapisho hayo yalitembelewa na watu mbalimbali" amesema Jaji.
Ameongeza " Mdai alisema pamoja na hayo machapisho yaliyochapishwa mpaka yanaonwa na mleta madai channel ilikuwa imetembelewa na Views 280.
" Malalamiko ya mleta maombi yanasema kwamba , mdaiwa alitamka kwamba yeye ni mla rushwa , mtu ambaye anatumia vibaya nafasi yake ambaye ni mtumishi wa umma na kusema mambo hayo siyo ya kweli " alisema Jaji Marlin.
Wadaiwa walikataa kuomba msamaha
Jaji huyo alisema kwamba mleta madai alileta madai waombe msamaha na wamlipe Bilioni 12 kama fidia ya uchafuzi wa hadhi yake na wamlipe Bilioni 1 kama adhabu kwa kile ambacho wamekifanya.
Alisema baada ya wadaiwa kupokea madai , mdaiwa wa kwanza na wa pili bila sababu za msingi walikataa kujibu madai hayo na hivyo kesi hiyo kuendelea bila wao kushiriki kwa vile walishindwa kujieleza .
Jaji Marlin alisema kwamba mdaiwa na 3 yeye alipata nafasi ya kujibu madai ya mdai . Alikubali yaliyoandikwa kwenye kielelezo namba 1,2,3, 4 na alipinga katakata kumchafua mdai.
" Mdaiwa alisema mdai hana sababu ya msingi ya kumburuza yeye namba 3 mahakamani na haoni sababu ya kuomba msamaha kwasababu hajahusika na kashfa hizo ambazo zinalalamikiwa.
Jaji alisema kwamba kesi ilivyofika tayali kusikilizwa mahakamani hapa mdai alikuwa na Wakili Kassim Mgilla, mdaiwa namba moja alikuwa na Wakili mmoja Hekima Mwasipu na mdaiwa namba tatu alikuwa na mawakili wawili ambao ni Ernest Mhagama, Tumsifu.
" Kama nilivyosema mdaiwa wa kwanza na wa pili hawakupata nafasi ya kujitetea kwakuwa wenyewe hawakutaka kujitetea.
Mashahidi waieleza mahakama
Kwa mujibu wa Jaji alisema shahidi Masiaga Msima amkazi wa Kata ya Manga ambaye ni mwanasiasa aliambia mahakama kuwa yeye anamfahamu mdaiwa wa kwanza japo hakushiriki kikao cha mbunge isipokuwa alisikia mbunge akitamka maneno ya kumshambulia Maswi kupitia YouTube channel ya Mara TV
Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa alipofuatilia ile TV ili awajulishe wengine juu ya mbunge anavyomshambulia mdai alikuta Mara TV imeondolewa mtandaoni. Shahidi alisema mdaiwa namba tatu hamfahamu isipokuwa anamfahamu kupitia taarifa zake mbalimbali kupitia channel yake ya Mara TV.
Shahidi huyo alisema kwamba aliposikiliza channel hiyo maneno mengine aliona yanaleta madhara na katika kikao hicho aliona watu zaidi ya 200 na mdaiwa wa kwanza aliongea maneno hayo kwenye YouTube na alijisikia vibaya kusikia maneno yenye maudhi .
Shahidi huyo aliiambia mahakama kwamba mbunge alisema mleta madai aliahidi kumjengea shule mkuu wa shule na alipofuatilia kwa mkuu wa shule kupata ukweli , mkuu wa shule hakuwa anamfahamu na wala hakuahidiwa kujengewa nyumba.
Shahidi alisema kwamba mdaiwa namba tatu kupitia Mara TV alionesha mbunge akimshambulia mleta maombi kwamba anapokea rushwa ,amejiandaa kuingia kwenye siasa amewahusisha makatibu wakuu wa Wizara mbalimbali anawadai pesa ili afanye shughuli zake za kisiasa kwa ajili ya kupata ubunge.
Jaji Marlin alisema kuwa shahidi wa pili Charles Kihengu ambaye ni mwanasiasa Katibu mwenezi wa Kata ya Manga alisema alishiriki kwenye kikao kilichohitishwa na mbunge.
Shahidi alisema kwamba mbunge alimshambulia kwa maneno ya kashfa kwa jila lake Maswi na kwamba badala ya kujadili mambo ya maendeleo yeye alianza kuongea mambo binafsi, kumshambulia Maswi kwamba anataka kutoa hela ili apate uongozi na alipofuatilia alibaini ni maneno ambayo yalikuwa sio ya kweli.
Shahidi huyo alisema kwamba mbunge Waitara alimshambulia mdai kuwa anajipitishapitisha , mdai ametengeneza makundi ili awawezeshe awape pesa kupitia makatibu wakuu ili wamwezeshe fedha wapate kumpigia kura.
Shahidi alisema alipofuatilia aligundua sio kweli na kwamba kama CCM kata walitoa taarifa katika uongozi wa juu wa chama .
Jaji alisema kwamba shahidi wa tatu Shirikisho Robart , yeye alisema anatoka chama pinzani kwamba alikuwepo kwenye mkutano wa mbunge.
Shahidi huyo alisema kwamba kuna maneno aliongea mazuri na mengine aliongea ya kumshambulia kwa jina lake kwamba mzee Maswi anatafuta pesa ili aende akatafute nafasi ya ubunge , na mkutano huo ulikuwa na watu zaidi ya 200.
Jaji wa Mahakama kuu alisema kwamba shahidi wa nne ambaye ni mdai Eliakim Maswi alisema kuwa wakati anashambuliwa kwa maneno ya kero na udhalilishaji alikuwa mtendaji mkuu wa PPRA kisha mh.Rais alimteua nafasi nyingine ya juu ya kuwa Katibu mkuu wizara ya katiba na sheria.
Shahidi alisema katika utumishi wake wa miaka 34 ameshika nyadhifa mbalimbali katika utumishi wa Umma . Tarehe 9/8/2023 , alipokea simu kutoka kwa rafiki yake akimwambia ameshambuliwa mtandaoni na usiku alishindwa kuangalia .
Alisema kesho yake asubuhi aliingia kwenye mtandao na kuona kichwa cha habari katika YouTube ya Mara TV 'Waitara Amjeruhi Maswi ' . Alichukua muda wa kutosha kusoma na kuona anayeshambuliwa ni yeye na taarifa ile ya video ilirushwa Mara TV YouTube .
Shahidi alisema aliyoyasikia yote yalikuwa ni mashambulio yenye kukera kwake na maneno hayo aliyasikia tarehe ,10, 8/2023 kupitia YouTube channel ya Mara TV na kwamba mbunge Waitara alimshambulia bila kuwa na ukweli wowote yaliyooneshwa na mdaiwa namba 2 na namba 3.
Shahidi alisema TV hiyo ilirusha maneno hayo bila hata kutafuta ukweli upande wa pili yaani hakubalance story.Hata hivyo alisema aliomba wadaiwa wote kuomba msamaha kwa kile walichokifanya lakini hawakufanya hivyo.
Shahidi alisema alifuatilia kujua TV hiyo inamilikiwa na nani kwa kufuatilia mamlaka ya usajili na kubaini Mara TV inamilikiwa na mdaiwa ambaye namba 3. Aliona yote yaliyosemwa kumuhusu yeye, alisema hayana ukweli wowote kwasababu yeye ni mteule wa Rais mpaka sasa.
Jaji alieleza kwamba Shahidi alisema kama ana tabia mbaya au kula rushwa asingeweza kuaminiwa na kuendelea kuteuliwa , alikana yeye sio mla rushwa na hawezi kutumia nafasi hiyo kuomba pesa makatibu wakuu kwa vile makatibu wakuu hawawajibiki kwake.
Alisema hata hivyo alipokuwa PPRA yeye alikuwa anaripoti kwa Katibu mkuu , hivyo isingekuwa rahisi yeye kuomba fedha ya rushwa kwa Katibu wake.
Kulingana na tuhuma hizo za rushwa shahidi alisema hajawahi hata siku moja kuitwa na TAKUKURU wala kuhojiwa na Katibu mkuu kiongozi kuhusu mambo hayo kwa vile yeye alikuwa mtumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Jaji Marlin ,shahidi alikana tuhuma kuwa si kweli kwamba yeye hana akili timamu na kwamba si kweli kwamba hathamini kazi yake bali anathamini kazi yake. Hivyo kutokana na matukio hayo yaliyofanywa na mdaiwa namba moja siyo ya kweli.
Shahidi alisema yamemdhuru sana yamemjeruhi katika utumishi wake wa umma na mbele ya watanzania wote, hivyo anaomba wamlipe fidia ya madhara hayo waliyomsababishia Tsh. Bilioni 12.
Pia alipwe fidia Tsh. Bilioni 1 kama adhabu kwa wadaiwa wote, kwakuwa yeye alijenga utu wake katika utumishi wa umma kwa miaka mingi hivyo adhabu hiyo inafanana na utu wake alioujenga kwenye utumishi wa umma.
Jaji wa Mahakama hiyo alisema kwamba baada ya upande wa kesi wa mlalamikaji kufungwa na mdaiwa namba tatu kujitetea akiongozwa na Wakili wake Mhagama .
Mahakamani yasikiliza video .
Jaji Marlin alisema kuwa iliposikilizwa Video iliyotekelezwa na mdaiwa namba tatu mdaiwa huyo alikataa kujihusisha na maneno yote na hivyo akaomba kesi hiyo iondolewe ina masuala ya kisiasa. Utetezi wake ulikuwa mfupi na alikataa katakata wakati wa maswali ya dodoso.
Alisema mdaiwa alikiri kukisikia kielelezo namba 3 (Clip) iliyochezeshwa mahakamani . Alisema aliyemuona anaongea kwenye kielelezo kile alikuwa ni mbunge Waitara na kwamba kimerushwa kupitia Mara TV yenye logo kulia na yeye aliiona.
Alisema Wakili wa mdaiwa huyo aliomba kupewa muda kuleta mawasilisho mahakamani na Wakili wa upande wa mdai ulikubali lakini hata hivyo mawasilisho hayakuletwa.
Jaji alisema kwamba mahakama hiyo imeongozwa na hoja 4 ikiwemo maneno yaliyotamkwa na mdaiwa wa kwanza ni kweli ni ya udhalilishaji? na kwamba mashahidi wote waliofika walisema maneno yaliyosemwa yalikuwa ya udhalilishaji yalimdhalilisha mdai.
Katika maneno yaliyotamkwa ya Video iliyochezwa maneno yalisemwa kuwa mleta madai hana akili timamu, hana heshima ya kazi, mleta madai anakusanya fedha ili aje kunitumia kwania ya kupata ubunge.
Jaji alisema maneno yaliyotamkwa yanaangaliwa ukweli wake je yametamkwa yana ukweli wowote au hayana ukweli wowote ?yawe yanalenga kushushia mtu heshima au hadhi yake yanaweza kuwa ya kutamka au kuandika.
" Kielelezo namba 3 kilipokelewa mahakamani hapa kinaeleza mdaiwa namba moja alitamka maneno yanayohusu mdai kuwa hana akili timamu na kwamba mdai ni mla rushwa. Sio jema katika jamii inafanya mtu aonekane siyo mtu mzuri ndani ya jamii.
" Mdaiwa alisema mdai anatafuta pesa ili aende kuhonga apate kiti cha ubunge wakati huo mleta maombi alikuwa ni mtumishi katika ngazi za juu kwa nafasi mbalimbali za uongozi . " alisema Jaji.
Aliongeza " Kumtaja afisa mkuu katika uongozi wa umma kwamba ni mla rushwa ni kumshushia hadhi yeye mwenyewe na nafasi anayoitumikia lakini pia kusema ana akili mbovu maana yake hata kazi anayofanya haimfai lakini akiendelea kubaki kwenye nafasi hiyo.
" Mahakama inaungana na mashahidi maneno yaliyosemwa na aliyetamka ni mbunge ambaye ni Mwita Waitara kwamba maneno hayo kwa ujumla wake yanakera ukizingatia nafasi aliyokuwa nayo mdai kwa wakati ule .
Alisema utetezi wa shahidi mmoja wa utetezi alieleza maneno yaliyotolewa ni kweli yalitamkwa na mbunge Mwita Waitara na yalilenga kumshushia hadhi mdai.
Alisema aliyerusha taarifa ni Mara TV, mdaiwa namba 3 alikiri Ile video ilirushwa kupitia chombo cha Mara TV. Hoja hiyo mahakama inaijibu ni kweli mdaiwa namba 2 na namba 3 walishiriki kurusha maneno ya kashfa maneno yaliyotamkwa na Mwita Waitara.
Kushoto ni Wakili Hekima Mwasipu, katikati ni Mwandishi wa Habari Karoli Jacob, na kulia ni Wakili Ernest Mhagama wakiwa katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma.
Mdai amepata madhara
Je mdai alipata madhara yoyote ? . Jaji Marlin alisema mdai ni mtumishi wa umma kwa muda mrefu kwa miaka zaidi ya 30, kumwambia kuwa hana akili vizuri ni kumdhalilisha na kuwadhalilisha watumishi wa umma .
Pia ni kuidhalilisha mamlaka iliyomteua maana yeye ana akili vizuri na ndio maana bado anafanya kazi na anaendelea kuaminiwa. Mpaka matamshi hayo yanatoka alikuwa ni mwajiriwa na mpaka sasa ni mwajiriwa.
" Hivyo sio kweli kwamba hana akili vizuri na sio kweli kwamba hana nidhamu kwa vile kwa maelezo ya mdai hajawahi kuonywa na mwajili wake wala kuitwa na mamlaka inayodhibiti masuala ya rushwa kuthibitisha kama anakula rushwa au la .
" Hii maana yake maneno yaliyotamkwa na mdaiwa wa kwanza hayakuwa na ukweli wowote hivyo yalikuwa ni maneno ya uongo yaliyolenga kushusha hadhi ya mdai hali ambayo imeaminiwa na mamlaka yake ya uteuzi ya mh. Rais kwa kumpa nafasi mbalimbali ikiwemo ya PPRA na bado anaendelea kuaminiwa kuwa Katibu mkuu wa wizara ya katiba na sheria." alisema Jaji.
Maneno yaliyosemwa ni ya kudhuru
Mahakama hiyo imejiridhisha kuwa maneno hayo yanaenda kumdhuru , kashfa zile zitaenda kumdhuru katika ajira yake lakini pia katika familia yake kwa vile ni baba mwenye mke ,baba mwenye mtoto.
Jaji alisema mdai alipotoa maelezo yake aliongea kwa hisia kali kwamba mdaiwa namba moja amedharau watumishi wa umma wote kwa vile yeye hajawahi kuwa mtumishi wa umma na hajui ni kwa kiasi gani watumishi wa umma wanavyojenga heshima zao katika jamii.
Jaji alisema pamoja na wadaiwa kutakiwa kuomba msamaha kama kielelezo namba moja kilicholetwa mahakamani hapa kinaonesha kwamba aliwaomba wadaiwa waombe msamaha lakini wadaiwa wote walikataa kuomba msamaha wakiamini waliyoyasema ni ya kweli.
Mdai amedhalilishwa
Jaji alisema wakati mdai yupo mahakamani walishindwa kuuliza maswali yaliyoonesha kwamba matamshi waliyoyatoa yalikuwa sio ya kumdhalilisha . Wadaiwa walishindwa kuleta ushahidi wa yale waliyoyasema kuhusu kura rushwa, kuhusu utovu wa nidhamu na kwamba mdai hana akili.
" Mdai alisema hajawahi kupelekwa hospitali kupimwa na kukutwa hana akili hivyo matamshi hayo ilikuwa ni kumdhalilisha .
Aliongeza kwamba mahakama hiyo imeona mdai alidhalilishwa . Je ni kitu gani wanastahili ? . Jaji alisema kuomba msamaha huo sio utetezi wowote isipokuwa kuomba msamaha kunafanya mtenda kosa aonekane amejutia kosa lake na inaweza mpunguzua adhabu.
" Wadaiwa katika kesi hii hawakuweza kuomba msamaha hivyo inaonesha walikuwa wamekusudia kutoa maneno ya kashfa hata baada ya kukumbushwa kwamba haikuwa sahihi walikataa kabisa kuyafuta maneno yake wala kuomba msamaha na hivyo kutoomba msamaha kunapelekea adhabu kuwa kubwa.
Fidia
Jaji alisema mdai katika hati yake ya madai ameomba malipo ya aina tatu . Malipo ya Bilioni 12 kama fidia kwa madhara aliyoyapata , Bilioni 12 kama fidia ya jumla, Bilioni moja kama fidia ya adhabu.
" Fidia ya madhara inatambulika kama fidia mahususi ambayo mdai anatakiwa kuthibitisha. Mleta madai yeye aliomba fidia ya jumla hakuthibitisha fidia ya madhara, hivyo mahakama imeona haina haja ya kuchambua kwa urefu fidia ya madhara .
" Fidia ya jumla ni hiari ya mahakama , mahakama ndio inapima ni wakati gani itoe fidia ya jumla kulingana na mwombaji na kesi iliyo mahakamani. Lakini katika kutoa fidia ya jumla mahakama ina vitu inavyotakiwa kuzingatia ukali .
" Kesi yetu hii ni ya matamshi ya kukera, matamshi ya kukashfu , ukweli wa matamshi yaliyotokea , ikiwa msamaha uliombwa , madhara ambayo mtu amekumbana nayo na madhara ambayo yanalenga kumuumiza haya yote yanaangaliwa na kufikiriwa katika Mahakama" alisema Jaji.
Alisema mlalamikaji ni mtumishi wa umma mpaka anafika mahakamani alikuwa hajawahi kuitwa TAKUKURU, alikuwa hajawahi kuonywa na Katibu mkuu.
Jaji alisema hata hivyo matamshi hayo yanaweza kuamsha mamlaka wakati wowote kutaka kujiridhisha kama yaliyotajwa au hayakutajwa. Alisema haijulikani ni wakati gani matamshi yale yatachukuliwa na mamlaka kuyafanyia kazi.
Alisema wadaiwa wote walishindwa kuleta ushahidi wowote kwa mwandishi au kwa mdomo kuhusu tuhuma walizozitaja dhidi ya mdai pamoja na kwamba waliopewa nafasi ya kufanya hivyo.
" Ni kweli matamshi yale yaliondolewa kwenye chombo cha habari ambacho waliposti , lakini hata hivyo bado kuna watu waliyasikia na bado kuna watu waliona hiyo video.
" Kwa vile umma ulisikia na hasa kwenye ule mkutano watu walienda na walisikia hadhi ya mdai imeharibiwa na kuathirika, mdai pia aliomba zuio wadaiwa wote kuacha Kumtaja kwenye vyombo vya habari au vyombo vingine vyovyote vya habari.
Hata hivyo mahakama ililidhia wadaiwa kutoripoti habari kuhusu mdai Eliakim Maswi huku wakihukumiwa wadaiwa wote watatu kulipa adhabu ya Bilioni 1, kulipa fidia ya jumla Bilioni 5 kwa madhara ambayo wameyasababisha.
Pia wadaiwa wote waombe msamaha hadharani na kwenye gazeti moja linalozunguka nchi nzima na walipe gharama za kesi.
Mei, 15, 2025 chombo hiki cha habari kiliripoti habari ya kesi hii namba 23 ya mwaka 2023.
Post a Comment