WANAFUNZI MWANALUGALI KUONDOKANA NA KERO YA KULA CHAKULA WAKIWA WAMESIMAMA
Na Gustaphu Haule, Pwani
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo kata ya Tumbi Halmashauri ya Mji Kibaha wanatarajia kuondokana na kero ya kula chakula wakiwa wamesimama na kukaa chini baada ya shule hiyo kupokea msaada wa fedha sh. Milioni 10.
Fedha hizo zimetolewa na taasisi ya fedha inayojihusisha na mikopo ya nyumba (TMRC)ambapo lengo lake ni kusaidia kutatua changamoto ya wanafunzi hao na fedha hizo ni kwa ajili ya ununuzi wa samani za bwalo la chakula la shule hiyo.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya fedha hizo yaliyofanyika shuleni hapo Juni 16, 2025 Mkuu wa shule hiyo Uyeka Kessy alisema kupatika kwa fedha hizo kumetokana na jitihada za mdau wa maendeleo Dkt.Charles Mwamwaja ambaye alifikisha mahitaji hayo kwa taasisi hiyo.
Afisa mtendaji Mkuu wa taasisi ya mikopo ya nyumba (TMRC)Oscar Mgaya ( Kulia )akipokea cheti cha heshima kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Kibaha Mjini na katikati ni Mdau wa maendeleo Dkt.Charles Mwamaja.
Amemshukuru mdau huyo wa maendeleo kwa kutafuta wafadhili ambao wamesaidia kutoa fedha hizo za kununua samani za bwalo la chakula huku akiomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kutatua vikwazo vya shule hiyo ikiwemo ujenzi wa uzio.
Mwenyeti wa bodi ya shule hiyo Alex Lubawa amesema kwasasa shule hiyo ina uhitaji wa uzio ambao utasaidia kudhibiti utoro kwa wanafunzi.
Mwenyekiti wa bodi ya Shule ya Sekondari Mwanalugali Alex Kubawa katika hafla ya kupokea fedha kwa ajili ya meza na viti za bwalo la chakula Shuleni hapo.
Naye Dk. Charles Mwamwaja ambaye pia ni Kamishna wa fedha kutoka Wizara ya Fedha na mkazi wa Kibaha Mwanalugali amesema amekuwa akiguswa na mambo ya maendeleo hususani yanayogusa jamii nzima.
Dkt.Mwamaja amesema wanafunzi wanatakiwa wasome katika mazingira rafiki ambapo ni pamoja na kuwa na sehemu nzuri ya kulia chakula, eneo la michezo na vyumba vya madarasa.
Mdau wa maendeleo Kibaha Mjini Dkt . Charles Mwamaja akiwa na wageni wake kutoka taasisi ya TMRC wakikagua Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Kibaha Mjini Leo Juni 16,2025.
Amesema mbali na kutatua changamoto ya bwalo hilo lakini pia ipo programu ya Safari yangu kielimu(SYK) ambayo itasaidia kuwajengea uwezo wanafunzi hao kujiamini kwa kuwakutanisha na watu ambao tayari wamefanikiwa ambao watatoa uzoefu wa maisha ya shule na namna walivyofanikiwa.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo Afisa Mtendaji wa taasisi hiyo ya TMRC Oscar Mgaya amesema zipo shule nyingi zenye mahitaji kama hayo na kwamba ujio wao umetokana na maombi kutoka kwa mdau wa maendeleo Dkt.Mwamaja.
Afisa mtendaji Mkuu wa taasisi ya mikopo ya nyumba (TMRC ) Oscar Mgaya kushoto akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh.milioni 10 Mjumbe wa bodi ya Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Kibaha Mjini Alex Lubawa (Kulia).
Mgaya amesema wameguswa na maombi ya shule hiyo ambapo taasisi imeamua kuchangia fedha kiasi cha sh. Milioni 10 zitakazotumika kutatua changamoto za shule hiyo ikiwemo kununua meza na viti kwenye bwalo la chakula.
Afisa mtendaji Mkuu wa taasisi ya TMRC Oscar Mgaya wa pili kutoka kushoto pamoja na mdau wa maendeleo Dkt .Charles Mwamaja wakitembelea Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Kata ya Tumbi Kibaha Mjini.
Bwalo la Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Kibaha Mjini ambalo wanafunzi wake wanakula kwa Kusimama na wengine kukaa chini.
Post a Comment