HEADER AD

HEADER AD

MAMA UKO TOFAUTI – 3


ENDAPO umeondoka, ni nadra sana kupoa,

Useme umeachika, ya kwamba unajitoa,

Ili waweze tunzika, hutaki wa kukuoa,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Hata eda haijesha, takuta mume aoa,

Aanza upya maisha, kama vile mpya ndoa,

Si watoto kuwavusha, kwenye mahitaji yao,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Afike mama wa kambo, huyo kwake mpya ndoa,

Wale waliopo shombo, ataka kuwaondoa,

Ili azipate tambo, na maisha yawe poa,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Watoto atesetese, na baba uone poa,

Badala ya uwaguse, mashaka kuwaondoa,

Amani kwao wakose, washindwe na kukohoa,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Watoto wawa yatima, jinsi wanawachokoa,

Hata ndoto zinazima, maisha yawapopoa,

Baba ameona vema, kuipata mpya ndoa,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Ungelikuwa ni mama, kama yaondoka ndoa,

Watoto wasingekwama, au baridi kuloa,

Na wao ungesimama, mengi ukiwaokoa,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Ndio maana nasema, wewe mama uko poa,

Kwako muhimu umama, kwa huo unajituma,

Ili uache alama, mema na si ya kuboa,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Zidi kuinuka mama, jinsi waijenga ndoa,

Na tena zidi kuvuma, watoto ukiwatoa,

Wakiwa watu wazima, tacheka na kukohoa,

Mama uko tofauti, watoto ukijaliwa.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments