PENDO LA MAMA LIPATE - 5
KULIKO wakose wote, na mtoto auawe,
Mwache mwenzangu apate, mtoto asiuawe,
Pendo la mama lipate, uzito lichukuliwe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Ilikuwa ni hukumu, mtoto abishaniwe,
Ubishi ulipodumu, kabidi uamuliwe,
Wamama wote wagumu, wanataka wasikiwe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Alolalia mtoto, litaka atambuliwe,
Alohai ni mtoto, ni wake wamuelewe,
Mwenye halisi mtoto, hakutaka amwelewe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Kitendawili kutega, utata utatuliwe,
Sulemani kawatega, mamtoto amwelewe,
Vizuri aliwakoga, kwamba mwana auliwe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Mtoto alopoteza, kafurahi auliwe,
Wote waweze poteza, na yeye afurahiwe,
Ndivyo alijieleza, mfalme amwelewe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Mtoto alomzaa, akataka asikiwe,
Akiuawa balaa, dunia imulewe,
Bora yeye kuchakaa, mama mwingine apewe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Sulemani kusikia, ilifanya aelewe,
Aliyemhurumia, mtoto wake mwenyewe,
Huyu akampatia, ili mwana alelewe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Ndiyo upendo wa mama, sisi sote tuelewe,
Hata vikikaza vyuma, mwana bora alelewe,
Kwake hana uhasama, hili na litambuliwe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Upendo wa Mungu kwetu, huo vema tuelewe,
Wala si wa mama zetu, uko juu tuelewe,
Ajali maisha yetu, hataki tuadhibiwe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Mungu atusaidie, Muumba tumuelewe,
Tena tumtumikie, dunia tusizidiwe,
Hadi tuje tufikie, milele tupokelewe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
Mama radhi ateseke, mtoto afanikiwe,
Akue na asifike, yeye tusimuelewe,
Watoto hilo lishike, wamama muwaelewe,
Mama kwa mtoto wake, hataki baya lolote.
(1 Wafalme 3:16-27)
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment