MAMA UZIDI KUDUMU - 2
PALE baba anakufa, wa kutegemewa mama,
Ila mama akikufa, kubaki na baba noma,
Ni ya mama maarifa, na watoto asimama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Pengine hajafa baba, kamtelekeza mama,
Ana watoto si haba, anabaki nao mama,
Hao wameshamkaba, hawezi waacha mama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Kazi zote zile baba, alizofanya za mama,
Hizo zaidi ya leba, zakula muda wa mama,
Ni jukumu anabeba, amwachie nani mama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Mama na wake watoto, kamwe hawezi wahama,
Kulea ni wake wito, jinsi anajisukuma,
Atauza hata vito, watoto waweze soma,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Sensa waweza pitisha, walo peke kinamama,
Ambao kwenye maisha, wamezaa kinamama,
Walipo wajikausha, wana waweze simama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Wengine wadogo sana, umri akinamama,
Mungu amewapa wana, kwao ndiko wajituma,
Kuolewa wanaona, kwa watoto hiyo noma,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Jinsi wanahangaika, kwa kazi wanachagama,
Hiki na kile washika, watoto waishi vema,
Sana wanachangamka, watoto wakisimama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Hao sana watongozwa, waolewe wanagoma,
Moyoni wanaongozwa, kwa watoto wawe mama,
Mapenzi yanapuuzwa, kwa sababu ya umama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Kama zile biashara, wanafanya kinamama,
Lengo ni maisha bora, watoto waweze soma,
Kwao iwe ni hasara, kwa watoto iwe vema,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Tunakushukuru mama, kwa watoto usalama,
Japo hiyo nzito ngoma, lakini unachagama,
Tena bila kulalama, washika wajibu mama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Mungu akutunze mama, wazidi kuita mama,
Hata kuwe na mlima, ng’ang’ana usijeggoma,
Kwako wapate egama, kwani kuna usalama,
Mama uzidi kudumu, kwako kuna usalama.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment