HEADER AD

HEADER AD

MAMA WA PEKEE MAMA - 1

HIVI nani kama mama, katika yetu dunia,

Ambaye anasimama, watoto kuangalia,

Unaye mwingine sema, tupate kuangalia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Aleaye mimba mama, miezi tisa timia,

Malezi mtoto mama, ndiye anamwangalia,

Kwa homa hata uzima, ndiye anamwangalia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Chakula watoto mama, ndiye anawapatia,

Wala hayuko salama, watoto kama walia,

Ni radhi yeye kukwama, watoto kifurahia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Akuombeaye mama, kutoka na kuingia,

Ili usije kukwama, katika yetu dunia,

Na wewe anasimama, hadi mwisho kufikia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Wazazi baba na mama, akilini waingia,

Kati yao hasa mama, watoto akumbatia,

Japo si sana avuma, kama walinganishia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Nyie mlio na mama, siri ninawaambia,

Mwangalie sana mama, aweze kufurahia,

Kumtelekeza noma, laana itawajia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Anayekupenda mama, mazuri akutakia,

Kwako hana uhasama, yote ukimfanyia,

Kwa kweli ni mwema mama, hana kulinganishia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Rafiki wa kwako mama, yote yako wamwambia,

Hata ukifanya noma, kwa upendo akwambia,

Hana uhasama mama, jinsi akusaidia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Wengine wakikuchoma, au kukushambulia,

Wa kukutetea mama, waziwazi awambia,

Waache kukusakama, sana anawakamia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Apewe maua mama, katika yetu dunia,

Jinsi anavyosimama, watoto aangalia,

Asingelikuwa mama, watoto ngeangamia,

Mama wa pekee mama, mwacheni aitwe mama.

Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments