UMEWAKUTA WATOTO WATUNZE KAMA WA KWAKO-4
MAMA huo si uzazi, hata ukiwa wa kambo,
Umeshaingia kazi, hebu acha zako tambo,
Fanya kazi ya ulezi, hao ndio lako jimbo,
Umewakuta watoto, watunze kama wa kwako.
Baba alipokuoa, ulishajua kitambo,
Kwamba mwanzo alioa, na watoto kwenye jimbo,
Vile wamuona poa, watoto sipige kumbo,
Umewakuta watoto, watunze kama wa kwako.
Mama wa kwao hayupo aliondoka kitambo,
Ndiwe mama uliyepo, hebu shikilia jimbo,
Iwe kama mama yupo, nawe wasiwe na jambo,
Umewakuta watoto, watunze kama wa kwako.
Kuna mifano kibao, wazuri mama wa kambo,
Walifanya kazi zao, si kuwapiga vikumbo,
Kupata maisha yao, wala vitamu kitambo,
Umewakuta watoto, watunze kama wa kwako.
Pale walipoolewa, jambo ni mama wa kambo,
Majukumu lielewa, watoto wale wa kambo,
Kwa wema walilelewa, bila ya zozote tambo,
Umewakuta watoto, watunze kama wa kwako.
Sasa watoto kukua, kwa yule mama wa kambo,
Mioyoni walijua, ni mama siyo wa kambo,
Moyo alivyofungua, bila kuwapa mafumbo,
Umewakuta watoto, watunze kama wa kwako.
Kwa sasa ya nchi mema, alaye mama wa kambo,
Sababu wa kwake wema, hakufanya baya jambo,
Ni watoto wanasema, hayo ni mazuri mambo,
Umewakuta watoto, watunze kama wa kwako.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment