MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA SHERIA
Na Gustaphu Haule, Pwani
KAIMU Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Nsajigwa George, amezitaka asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, uwazi na uwajibikaji ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa jamii.
Nsajigwa ametoa kauli hiyo Juni 26,2025 wakati akifungua mkutano wa jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Pwani uliofanyika katika Ukumbi wa mdogo wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani George Nsajigwa akizungumza katika kikao cha mashirika yasiyo ya kiserikali Juni 26,2025 Mjini Kibaha.Katika hotuba yake Nsajigwa amesisitiza umuhimu wa mashirika hayo kuzingatia taratibu za kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi, naomba niagize kuwa mashirika yote yafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni,msibadilike na kuwa sehemu ya migawanyiko ya kisiasa au uchochezi na Serikali inawategemea katika kulinda amani na utulivu, ambayo ni tunu ya taifa,” amesema Nsajigwa.
Aidha, ameeleza kuwa mashirika hayo ni wadau muhimu wa Serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo, kuimarisha ustawi wa jamii, na kutekeleza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na mikakati ya kupunguza umaskini.
Katika hatua nyingine Nsajigwa amemuagiza msajili msaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Pwani Grace Tete, kuhakikisha anakusanya changamoto, mapendekezo na michango ya mashirika hayo kwa lengo la kuyafanyia kazi kwa pamoja ili kuboresha utoaji wa huduma zenye tija.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ambaye pia ni afisa ufuatiliaji na tathmini mkuu kutoka ofisi ya msajili wa NGOs, Charles Komba, amesisitiza umuhimu wa utoaji wa taarifa sahihi za kifedha na idadi ya walengwa waliowafikiwa kwenye ngazi ya mkoa, pamoja na kujenga uhusiano thabiti na wafadhili.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Charles Komba akizungumza katika kikao cha mashirika yasiyo ya kiserikali kilichofanyika Juni 26,2025 Mjini Kibaha.“Serikali imetambua umuhimu wa mashirika haya na imeweza kuandaa miongozo mbalimbali ikiwemo mwongozo wa mchango wa NGOs, pia ushirikishwaji wao katika vikao vya ngazi ya Kata, Wilaya na mkoa, pamoja na kuandaa mfumo wa usajili wa kielektroniki wenye ufanisi zaidi,” amesema Komba.
Naye mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Pwani, Prisca Ngweshem, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa na kuahidi kuendeleza mashirikiano hayo hususan katika utoaji wa elimu kwa jamii, huduma bora na takwimu sahihi, ili kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Pwani Prisca Ngweshem akizungumza katika kikao cha mashirika yasiyo ya kiserikali kilichofanyika Juni 26, 2025 Kibaha Mjini.
Post a Comment