MITARA NI NINI
?
MITARA ni mila gani? Nijuzeni wahisani,
Nami nataka baini, wasiwasi nitoeni,
Majibu nipatieni, yenye vina na mizani.
Mitara ni mila gani? Nami nataka bayana.
Hili neno siyo geni, linanichoma moyoni,
Asili yake ni nini? Ndugu nifahamisheni,
Maana sijabaini, moyo wangu mashakani.
Mitara ni mila gani? Nami nataka bayana.
Si leo, tangu zamani, mitara limesheheni,
Faida yake ni nini? Tafadhali nijuzeni,
Nauliza kwa huzuni, msifikiri utani.
Mitara ni mila gani? Nami nataka bayana.
Imani yangu ni duni, kusema si mshindani,
Majibu nitumieni, andikeni kiundani,
Wajuzi jiridhisheni, mboni zangu fumbueni.
Mitara ni mila gani? Nami nataka bayana.
Wadau niteteeni, msiniache pembeni,
Gizani niondoeni, mwangani nipitisheni,
Nishikeni mikononi, salama nifikisheni.
Mitara ni mila gani? Nami nataka bayana.
Naelekea mwishoni, rafiki nawathamini,
Kujua ninatamani, fumbo nifumbulieni,
Semeni kwa umakini, Kiswahili tumieni.
Mitara ni mila gani? Nami nataka bayana.
Mtunzi: Sir Dody, Mudio Islamic Seminary School, Kilimanjaro, 0675 654 955 / 0762 396 923
Post a Comment