VIJANA WATAKIWA KUTOTUMIKA OVYO
Na Gustaphu Haule, Pwani
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Kwakibosha kilichopo Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo ,mkoani Pwani Shaban Athumani, amewataka vijana kuacha kutumika na watu wachache wenye nia ovyo ya kutaka kuharibu amani na utulivu hapa nchini.
Athumani ametoa wito huo katika mdahalo maalum wa kuwajengea uwezo vijana juu ya kukabiliana na vitendo viovu sambamba na kuwahamasisha vijana kulinda amani ya Taifa iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mdahalo huo umefanyika Juni 14, 2025 katika Kitongoji hicho na kuwashirikisha vijana zaidi ya 500 kutoka makundi mbalimbali wakiwemo bodaboda,mama lishe ,wapaka rangi na hata vijana kutoka UVCCM.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwakibosha kilichopo Kata ya Mapinga MBagamoyo Mkoani Pwani Shaban Athumani akizungumza katika mdahalo wa Vijana kuhusu kulinda amani ya Taifa uliofanyika Juni 14,2025 katika Kitongoji hicho.
Amesema kuwa mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu unaokwenda kuwaweka madarakani viongozi akiwemo Rais, Wabunge na Madiwani na hiyo ndio fursa kwa vijana kuchagua viongozi wanaowataka.
Amesema badala ya vijana kukaa na kuwaza namna ya kutumia fursa ya kuwapata viongozi hao unakuta wapo vijana waanza kuingia katika makundi ya ovyo yanayotumika na watu wachache kwa lengo la kuharibu tunu ya amani iliyopo nchini.
"Wapo waharifu wengi wamekuwa wakiwatumia vijana kuharibu Taifa letu lakini mimi hapa Kibosha nimejipanga kuhakikisha nawafanya vijana wawe nafikra za kulinda Taifa lao na sio kununuliwa,"amesema Athumani
Athumani ameongeza kuwa wapo watu wachache wenye fedha wanawatumia vijana kusukuma ajenda zao kwahiyo lazima wakati mwingine wakumbushane wajibu ili kulinda amani ya Taifa.
"Kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye uchaguzi Vijana hakikisheni mnamkataa mtu yeyote mwenye dhamira mbaya ya kutaka kuchafua na kuharibu amani,utulivu na usalama wa Nchi yetu ,msikubali kutumika ovyo Kwa maslahi ya mtu mmoja,"amesema Athumani
Ameongeza kuwa, Tanzania ndio nchi pekee yenye amani kuliko mataifa mengine duniani na inaonekana wazi kuwa nchi hizo kila siku wanapigana vita kwahiyo ni lazima vijana wajitoe kulinda amani.
" Vita ikiingia Tanzania hatutakuwa na sehemu ya kukimbilia na tunaona huko Nchini Kongo, Sudan na kwingineko ambako amani imetoweka na watu wake wanatafuta pakukimbilia ,je sisi tutaenda wapi? amesema Athumani akiwahoji vijana hao
Kuhusu fursa za kiuchumi, amesema kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kiuchumi lakini shida ni namna ya kuzitumia fursa hizo lakini umefika wakati vijana wanatakiwa kujitafakari juu ya raslimali walizonazo.
Fursa mojawapo ni upatikanaji wa ardhi kwa bei nafuu,Maji ya kutosha ,bahari ,mito na mabonde ya kutosha ambapo vijana wanaweza kujikita katika Kilimo,ufugaji, uvuvi, useremala kwa ajili ya kukuza uchumi wao.
Katika mdahalo huo mada tatu zilifundishwa ikiwemo mada ya Mtazamo wa Vijana wa sasa katika kulinda Taifa la Tanzania,Fursa zilizopo katika ujenzi wa uchumi wa Taifa la Tanzania pamoja na wajibu wa viongozi katika kuboresha maisha watu wanaowaongoza
Mkufunzi wa mhadalo huo Mwalimu Hajj Karanje ambaye alianza kufundisha mada ya kwanza amewaambia vijana waache mitazamo ya kuwashambulia viongozi na badala yake wawashauri nini chakufanya ili kujenga uchumi na kuleta Maendeleo ya sehemu husika.
Mkufunzi wa mdahalo wa Vijana katika Kitongoji cha Kwakibosha uliofanyika Juni 14,2025 Haji Karanje(kushoto) na Kulia ni mwenyekiti wa Kitongoji hicho Shaban Athumani.
Karanje,amesema kuwa wamekuwa na tabia ya kumshambulia kiongozi pale anapokosea jambo ambalo sio sahihi na kwamba wanapaswa kumshauri kiongozi wao kufanya jambo jema kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo, Mohamed Omary mshiriki wa mdahalo huo amemshukuru mwenyekiti wa Kitongoji hicho Shaban Athumani kwa kuandaa mdahalo huo kwani unawasaidia kuwakumbusha wajibu wao lakini ameomba wanapopewa mafunzo kama hayo Serikali ikumbuke kuwapa nyenzo za kufanyiakazi za kujiongezea uchumi.
Vijana wa Kitongoji cha Kwakibosha kilichopo Kata ya Mapinga Bagamoyo Mkoani Pwani wakishiriki mdahalo wa kulinda amani ulioandaliwa na Mwenyekiti wao Shaban Athumani Juni 14,2025.
Post a Comment