HEADER AD

HEADER AD

ZIKO WAPI ZAMA ZETU?

ZIKO wapi zama zetu, zama zile za zamani,

Enzi zile nyumba zetu, tunaketi sebuleni,

Sehemu ya kukaa tu, jamaa na majirani,

Leo hii nyumba kubwa, lakini hazina watu.


Vile vyumba vidogodogo, vya kule kwetu nyumbani,

Tulikosogoa sogo, na hata mwingi utani,

Zilikuwa nyumba ndogo, sebule hata vyumbani,

Leo hii nyumba kubwa, lakini hazina watu.


Ni ardhi na kuta tu, ndio zajaa nyumbani,

Hata varanda kubwa tu, vitofali vyasheheni,

Ni mbwa wanabweka tu, husogei varandani,

Leo hii nyumba kubwa, lakini hazina watu.


Zamani chakula chetu, tulichokula nyumbani,

Kilitoka shambani tu, kikapikwa mafigani,

Mikeka majamvi yetu, palikuwa ni mezani,

Kwa leo chakula chetu, ukisasa watawala.


Mihogo na ndizi zetu, dagaa toka mtoni,

Wali ugali kwa watu, tulimimina tumboni,

Kwenye masinia yetu, tukila na majirani,

Kwa leo chakula chetu, ukisasa watawala.


Zile sufuria zetu, zapotea duniani,

Sasa hotpot zetu, na minofu ya sokoni,

Imejaa nyumba zetu, kila mtu na sahani,

Kwa leo chakula chetu, ukisasa watawala.


Enzi hata shule zetu, likuwa sawa nchini,

Kwa hiyo wazazi wetu, walikuwa furahani,

Tulisema twende zetu, kuongozana shuleni,

Leo hii nyumba kubwa lakini hazina watu.


Mchakamchaka wetu, siyo sasa ni zamani,

Hata zile namba zetu, usichelewe shuleni,

Haziko kwa shule zetu, akademi ziko ndani,

Leo hii nyumba kubwa, lakini hazina watu.


Uwani kwa babu yetu, kwa hadithi za zamani,

Sasa hivi siyo kwetu, kinababu wa shimoni,

Na wale walio kwetu, wamekaa kizamani,

Leo hii nyumba kuwa, lakini hazina watu.


Na zile hadithi zetu, lifunza mengi kichwani,

Na tena kwa raha zetu, kicheko kingi uwani,

Watoto jirani zetu, lifika pia nyumbani,

Leo hii nyumba kubwa, lakini hazina watu.


Maisha sasa si yetu, kama tuko ugenini,

Yetu hatujui katu, bali mengi ya kigeni,

Hata lugha zawa butu, kusema ni kizamani,

Leo hii nyumba kubwa, lakini hazina watu.


Kule kulikuwa kwetu, kumeshatoka usoni,

Kwa sasa wala si kwetu, ni kujifungia ndani,

Ni mageti kila mtu, afanyacho hukioni,

Leo hii nyumba kubwa, lakini hazina watu.


Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments