SERIKALI YATAKA USHIRIKIANO KUKOMESHA RUSHWA NCHINI
Na Samwel Mwanga,Simiyu
SERIKALI imewataka wananchi na wadau wa maendeleo hapa nchini kushirikiana kwa dhati katika mapambano dhidi ya rushwa, na sio kuiachia tu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimentu ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,George Simbachawene amesema hay o , jumanne , Juni 10,2025 mjini Bariadi wakati wa uzinduzi wa jengo la kisasa la ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Simiyu.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimentu ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,George Simbachawene akizungumza kabla ya kuzindua jengo la TAKUKURU mkoa wa Simiyu.Amesema kuwa rushwa ni kansa inayodhoofisha ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa,hivyo kila mtanzania anapaswa kuwa sehemu ya mapambano hayo.
."Rushwa inapofusha. Ili tuwe na jamii yenye ustawi, ni lazima kupambana na kansa ya rushwa kwa juhudi za pamoja bila kudharau hata rushwa ndogo.
“Rushwa ndogondogo ni mbaya sana, zinaumiza wananchi na ni kero katika maeneo ya huduma kama polisi, vituo vya afya, masoko na taasisi nyingine za jamii," amesema.
Amesema kuwa ni vizuri kwa viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kukemea vitendo vya rushwa kwa kuwa wanao wajibu wa kuhubiri maadili na kuwajenga waumini kuwa wazalendo wanaoepuka kuhusika au kushiriki katika vitendo hivyo.
Waziri Simbachawene amesisitiza kuwa serikali inaendelea kushughulikia kero mbalimbali za wananchi, hasa zile zinazochochea mazingira ya rushwa.
Akiwaelekeza watumishi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa, hasa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwezi oktoba mwaka huu.
"Mapambano ya rushwa hayawezi kufanywa na Takukuru pekee, tukishirikiana wote, tutaweza kumpambana adui huyu,natoa rai kwa viongozi wa dini, tumieni misikiti na makanisa kufundisha waumini madhara ya rushwa," amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU nchini, Chrispin Chalamila,amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, ili taifa liendelee kuwa mahala salama na pa haki kwa wote.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Chrispin Chalamila,akizungumza kabla ya uzinduzi wa jengo la Takukuru mkoa wa Simiyu mjini Bariadi.Naye Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Simiyu, Manyama Tungaraza, amesema kuwa jengo jipya la ofisi hiyo limekamilika kwa gharama ya TSh Milioni 640 likiwa na lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.
Amesema kuwa taasisi hiyo mkoani humo imejikita zaidi kwenye uzuiaji wa rushwa kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu katika miradi ya maendeleo, ambapo wananchi wamekuwa wakieleza kero mbalimbali zenye viashiria vya rushwa.
"Kupitia madawati yetu ya uchunguzi, elimu kwa umma, uzuiaji na huduma za kisheria, tunapokea na kushughulikia malalamiko kwa ufasaha.
“ Wananchi wameendelea kuibua changamoto ambazo tukiziachia zinaweza kuchochea vitendo vya rushwa, ushirikiano wetu na wadau umekuwa muhimu sana katika kutoa majibu ya kero hizo," amesema.
Uzinduzi wa jengo hilo umepokelewa kwa matumaini mapya ya kuongeza kasi na ufanisi wa Takukuru mkoani Simiyu katika mapambano dhidi ya rushwa, hususan katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
Jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Simiyu .
Post a Comment