TUWAPE THAMANI YAO
TUWAPE yao heshima kina mama duniani,
Kwa upendo na huruma, tuwape yao thamani,
Na mengi wanasimama, wapambana kwa yakini,
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
Wajituma si utani, kuzilea familia,
Si leo tangu zamani, makuzi huzingatia,
Kulea hawajivuni, watoto hufurahia,
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
Wamebeba majukumu, nayosema si utani,
Hilo sote twafahamu, wanawake washindani,
Hakika tuwaheshimu, wanawake duniani
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
Wametoka utumwani, tofauti na zamani,
Wengi wapo makazini, wajuzi na wenye fani,
Wamejitoa gizani, mejisogeza mwangani,
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
Wengine ni viongozi, na wengine marubani,
Wapo wale watetezi, wabobezi wenye fani,
Kazi yao utetezi, ni wengi mahakamani,
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
Na tunaye jemedari, rais wa Tanzania,
Ni mwanamke jasiri, apewe yake maua,
Kwakuongoza hodari, Rais mama samia,
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
Wengine ni mawaziri, bungeni wametulia,
Wapo pia wahariri, nchini wameenea,
Na wapo wanahabari, kwa hilo twajivunia,
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
Heri tunawatakia, wanawake duniani,
Shairi ninalitoa, nimefika ukingoni,
Mengi mmeyasikia, wanawake hongereni,
Tuwapende kina mama tuwape yao thamani.
SirDody (_Mudio high school)
Kilimanjaro , 0762396923 ,0675654955
Post a Comment