HEADER AD

HEADER AD

VYAKULA VYENYE VIRUTUBISHI LISHE KUUKABILI UDUMAVU SIMIYU


Na Samwel Mwanga, Maswa

JAMII katika mkoa wa Simiyu imeshauriwa kuondoa mitazamo tofauti kuhusu vyakula na mafuta vinavyoongezwa virutubishi ili kuondokana na changamoto za lishe katika mkoa huo wenye idadi kubwa ya watoto wenye udumavu.

Hayo yameelezwa jumatano,Juni 11,2025 na Afisa kutoka Wizara ya Afya,Idara ya kinga, sehemu ya huduma za lishe, Haliye Abubakary wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Sangamwampuya na Chugamita wilaya ya Maswa kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kukabiliana na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano.

     Afisa kutoka Wizara ya Afya,Idara ya kinga,sehemu ya huduma za lishe,Haliye Abubakary (kulia) akizungumza na baadhi ya wakinamama wa kijiji cha Sangamwampuya mara baada ya kunywa uji ulioongezwa virutubishi.

Ukubwa wa tatizo la udumavu katika mkoa huo umeelezwa kuongezeka huku taarifa mpya zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zikionesha kati ya watoto 100 wenye miaka chini ya mitano, 33 wana changamoto hiyo.

“Hali ya udumavu katika mkoa wa Simiy inazidi kuongezeka kwani takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2016 watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu walikuwa asilimia 32 na idadi imeongezeka kwa mwaka 2024 imefikia asilimia 33.4 na kuacha maswali mengi kwa kuzingatia kwamba mkoa huu ni moja ya mikoa inayozalisha kwa wingi vyakula vya aina mbalimbali,”amesema.

Amesema kuwa katika kukabiliana na hali hiyo serikali imeamua kufanya kampeni kwa kushirikiana na sekta binafsi ambayo ni kampuni  inayojihusisha na uboreshaji wa lishe(SANCU) ili kusaidia katika kampeni hiyo.

Ofisa lishe wa mkoa wa Simiyu,Dk Chacha Magige amesema mitazamo inatofautiana kwenye jamii kuhusu vyakula vinavyoongezwa virutubishi,wapo wanaoelewa na  kuvitumia lakini wapo ambao hawana uelewa wa kutosha,ambao wanapingana na ndicho chanzo cha udumavu kwa watoto.

       Afisa lishe mkoa wa Simiyu,Dk Chacha Magige akieleza hali ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano katika mkoa huo.

Amesema kuwa mkoa huo umeweka mipango ili kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo ya kuongeza virutubishi kwenye vyakula na hasa katika unga wa mahindi ambao unatumika katika chakula kwenye familia na shule.

“Hali ya udumavu katika mkoa wa Simiyu iko juu kwani kati ya watoto 100 wapo watoto 33 ambao wanakabiliwa na tatizo la udumavu,ni hali ambayo inatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka na kwa nguvu kubwa ili kuwanusuru watoto hao.

“Na tunasisitiza chakula cha wanafunzi katika shule na familia ni lazima unga wake uongezwe virutubishi na sasa tuna mradi wa kufunga mashine ambazo zitasaidia kuchanganya unga wa mahindi na virutubishi,”amesema.

Amesema kuwa unga ambao umeongezewa virutubishi hauna changamoto zozote za kiafya kama baadhi ya watu wanavyoamini bali zina virutubishi vyote muhimu katika kukabiliana na utapiamlo na udumavu.

Eliamani Mmari ni mwakilishi wa kampuni ya SANCU amesema kuwa wamejikita kuongeza virutubishi katika unga wa mahindi kwa lengo la kuimarisha afya za walaji .

" Ila kwa sasa wamebaini ya kuwa watoto walio wengi wamekuwa na changamoto ya afya kwa kuzaliwa kwa kutokamilika kutokana na kuwa na mgongo wazi,vichwa vikubwa pamoja na mgongo sungura kunakosababishwa na wazazi wao hasa akina mama kutokula vyakula ambavyo havina virutubishi " amesema.

Mayombi Emanuel ni mkazi wa kijiji cha Sangamwampuya amesema kuwa baadhi ya watu wanaopinga kutumia unga wa mahindi uliongezewa virutubishi kwa madai kuwa unapunguza nguvu za kiume.

      Baadhi ya wananchi katika kijiji cha Sangamwampuya wakipatiwa uji ulioongezwa virutubisho.

“Wale ambao hawana elimu wanapingana nayo wakidai watashindwa kuzaa au kupunguza watu lakini wakielimishwa wataelewa tu .

Esther Bassu ni mkazi wa kijiji cha Mbugamita amesema kuwa umasikini wa kipato na ukosefu wa elimu kuhusu lishe sahihi kwa wazazi hasa wakina mama.

“Elimu ya lishe huku maeneo ya vijijini ni wachache sana ambao wanaifahamu na ndiyo maana udumavu unakuwepo kutokana na kula chakula cha aina moja tu mara kwa mara ili tuweze kufanikiwa ni lazima elimu hiyo itolewe kwa nguvu zote,”amesema.

Naye Agnes Azami mkazi wa kijiji cha Sangamwampuya amesema kuwa ushirikiano wa sekta binafsi na serikali katika uzalishaji wa vyakula vyenye virutubishi ni jambo la msingi ili kukabiliana na udumavu.

 


No comments