HEADER AD

HEADER AD

WAJUKUU WA KIUME, BIBI AMEWAPANIA-2

WAJUKUU wa kiume, bibi amewapania,

Na midomo msiume, ni jinsi awazimia,

Anachotaka mkome, mademu papatikia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Si kila mnachotaka, mwaweza kujipatia,

Mkishindwa kukishika, sipaparike tulia,

Kupata kukosa shika, ndiyo mwendo wa dunia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Hatuishindi tamaa, kuzidi ikumbatia,

Kufanya hivyo balaa, watu tutajitakia,

Ni sawa na ukichaa, makali kushikilia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Tamaa kuendeleza, ni ujinga nakwambia,

Hapo mwisho kuteleza, na pua kuangukia,

Badaye takapowaza, utabakia walia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Hili nalo la muhimu, vema lipate ingia,

Kila tuonacho humu, na hata kukitumia,

Wala nasi hakidumu, dunia twaiachia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Hivyo vyote uonavyo, si vyote vya kutumia,

Uviache hivyohivyo, macho yakufurahia,

Kutaka vyote wa hovyo, somo halijaingia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Kikusubiricho sanda, watayokufunikia,

Hiyo nayo utakwenda, pale utapoishia,

Hivyo polepole nenda, vitu kuvikurubia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Na hii muhimu sana, bibi anakuambia,

Mjukuu akuona, unajihangaikia,

Wanawake ukiona, unataka wazukia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Heshima yako kidume, sivyo unafikiria,

Ulambe wengi kidume, tuweze kukusifia,

Hata vipi ujitume, huko wajiharibia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Hivi wapi lisikia, mtu wanamsifia,

Jinsi alijilambia, wanawake Tanzania,

Au mwanamke pia, alivyoruka na njia?

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Thamani yako sikia, mwanaume akwambia,

Sio uume sikia, jinsi unautumia,

Fimbo ya kuangamia, mbali huwezi fikia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Kwa huo uza thamani, katika yetu dunia,

Ukose katika dini, vile tunaisikia,

Na maisha yawe duni, hata uwe na dunia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Hadhi uwajibikaji, na staha nakwambia,

Utulivu mshikaji, ngazi utajipandia,

Hivyo kwako ni mtaji, hata Mungu kumwingia,

Bibi na kanuni zake, ni vema kuzingatia.

Mtunzini  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments