HEADER AD

HEADER AD

RC PWANI ATAJA MIRADI ITAKAYOZINDULIWA NA RAIS SAMIA

NA Gustaphu Haule, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema maandalizi ya uzinduzi wa Bandari Kavu katika eneo la Kwala unaotarajia kufanywa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Julai 31,2025 yanaendelea vizuri.

Kunenge ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Julai 30,2025 mara baada ya kutembelea na kukagua maandalizi ya uzinduzi huo katika maeneo yote muhimu.

Amesema mkoa umejipanga vizuri katika kupokea ugeni huo ambapo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali ombi la kuwa mgeni rasmi kwakuwa anafahamu ratiba zake ni ngumu.

        Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa habari katika Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Kibaha Vijijini Julai 30,2025.

Amesema kuwa Rais Samia akiwa katika eneo la Kwala atafanya shughuli mbalimbali ikiwemo  kuzindua safari rasmi safari  ya treni ya Mwendokasi (SGR) ya kubeba Makasha na kuzindua bandari Kavu ya Kwala .

Pia Rais ataweka jiwe la msingi katika Kongani ya viwanda itakayokuwa na viwanda 250 na kwamba mpaka sasa tayari viwanda Saba vimekamilika na vingine vinne vipo katika hatua ya ujenzi.

Kunenge amesema bandari Kavu ya Kwala itaongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ambapo kimsingi bandari Kavu hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa Makasha katika bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 30.

Amesema eneo la Bandari Kavu ya Kwala itaileta nchi za Afrika pamoja zaidi ya 11 na kwamba mpaka sasa nchi tisa tayari  zimeanza mchakato wa kujenga bandari Kavu kwa ajili ya nchi zao ambapo ametaja nchi hizo kuwa ni 
 Kongo, Zambia,Burundi,Malawi, Zimbabwe na Uganda ambapo pia alisema Sudan na Somalia nao wameonyesha nia .

       Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akipokea maelezo ya maandalizi ya uzinduzi wa Bandari Kavu ya  Kwala kutoka kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Moses Magongwa utakaofanyika Julai 30,2025.

" Kupitia Bandari hiyo itakuwa sehemu ya kuongeza uchumi kwa Wakazi wa maeneo ya mkoa wa Pwani wanaopitiwa na barabara ya Bandari Kavu na pia itakuwa sehemu ya kuongeza ajira kwa vijana.

" Jambo kubwa la msingi ni kuwa Pwani imepata nafasi ya kuonyesha namna Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ilivyofanya mambo makubwa na kwamba hilo linapaswa kufahamika na duniani pamoja na mikoa yote nchini Tanzania " amesema. 

Hata hivyo, Kunenge ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Pwani pamoja na maeneo mengine ya karibu kujitokeza katika kushirikiana na Rais Samia katika ziara hiyo kwakuwa maandalizi ni mazuri na upo utaratibu wa kuhakikisha Kwala inafikika kirahisi.
        Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akikagua maandalizi ya uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala leo Julai 30,2025 , uzinduzi huo utafanyika kesho ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

No comments