HEADER AD

HEADER AD

KINA MANDELA NI WENGI - 1

HII Afrika Kusini, taifa la duniani,

Huko ziko nyingi dini, watu wake waamini,

Zingine ni za nyumbani, na zingine za kigeni,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Ni Nelson Mandela, kajaa masikioni,

Harakati si usela, zamuweka kileleni,

Kama kura siyo kula, mabingwa wengi Kusini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Lipigania uhuru, akatiwa gerezani,

Akatoka kawa nuru, huko Afrika Kusini,

Sasa nchi iko huru, inapepea amani,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Aprili shinasaba, twaijua duniani,

Tisina nne si haba, kongwa likapigwa chini,

Dhuluma kapigwa roba, uhuru kote nchini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Madikizela Mandela, huyu mama yetu Winnie,

Wala hakufunga tela, alivyokuwa vitani,

Huyu mke wa Mandela, mama taifa nchini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Lipambana sana huyu, wengi kiwa gerezani,

Wabaguzi kwake huyu, likuwa mwiba machoni,

Jela alifungwa huyu, akiwa ukombozini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Mpiganiaji haki, wa huko kwake nchini,

Nafasi anamiliki, heshima kubwa barani,

Wengi tunamlaiki, Mama Afrika Kusini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Na Webster David, msomi kule kusini,

Alileta ukaidi, akiwa bado shuleni,

Kupinga kwa makusudi, ubaguzi michezoni,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Na Helen Suzman, mpiganaji kusini, 

Alipokuwa Bungeni, alikuwa ni makini,

Haki kwake mdomoni, alikuwa ni vitani,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Miaka kumi na tatu, alisimama aloni,

Kweli weupe si watu, walimcheka jamani,

Hakubabaika katu, kitaka haki nchini,

Uhuru wan chi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments