HEADER AD

HEADER AD

KINA MANDELA NI WENGI - 2

>>Solomon Mahlangu mpiganaji makini

SOLOMON Mahlangu, mpiganaji makini,

Na Mandela wanguwangu, waliingia vitani,

Shule yake Mahlangu, aliingia mitini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Miaka ishinatatu, alikuwa maishani,

Alifanya vingi vitu, huko Afrika Kusini,

Huyu ni shujaa wetu, aingie akilini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Alijifunzia jeshi, Angola ughaibuni,

Umkhonto we Sizwe jeshi, akapigane nyumbani,

Mpiganaji mbishi, aliyefia kazini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Wakiingia nchini, walishukiwa njiani,

Mbio za vichochoroni, kuwaweka hatarini,

Watu wawili njiani, risasi tele mwilini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Na hakuhusika katu, watu kwenda mautini,

Akanyoshewa mtutu, kisha akawekwa chini,

Mashtaka yenye kutu, yakasomwa kortini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Alihukumiwa kifo, na kunyongwa hadharani,

Hakusababisha vifo, ubaguzi wa Kusini,

Kunyongwa kikawa kifo, mpiganaji jamani,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Maneno yake ya mwisho, yamebaki vitabuni,

Na tena ni uamsho, bara hata visiwani,

Yamebaki ukumbusho, kwa Afrika Kusini.

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

Waambie watu wangu, ya kwamba nawapendeni,

Na ya kwamba damu yangu, yamwagie ardhini,

Mti wa matunda yangu, ni ukombozi kusini,

Uhuru wa nchi hiyo, kina Mandela ni wengi.

  >>Solomon Mahlangu mpiganaji makini

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments