KINA MANDELA NI WENGI - 3
>> Steve Biko - Anakumbukwa daima
Steve Biko muone, maarufu Afrika,
Kazi yake tuione, kukomboa Afrika,
Alimwaga lake tone, haki aweze simika,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Kwa kupinga ubaguzi, sauti ilisikika,
Walakini wabaguzi, wakaweza kumshika,
Tunajua waziwazi, aishi hawakutaka,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Katika mahojiano, polisi lipomshika,
Hatukusikia neno, akawa ametoweka,
Tulisikitika mno, maishaye kukatika,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Eti hospitalini, polisi walisikika,
Alifikwa mautini, wakiwa wamemshika,
Ghadhabu ya duniani, bado haijakatika,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Biko lianzisha SASO, chama kilichotukuka,
Ni cha wanafunzi yoso, kunyanyaswa walichoka,
Walilani manyanyaso, walopata Waafrika,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Kile chama BCM, na hicho kiliundika,
Nguvu yake twafahamu, jinsi kiliwajibika,
Vile vyama vya muhimu, ndani havikusikika,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
BCM kilipanga, na kazi ikapangika,
Ubaguzi kuupinga, uhuru uweze fika,
Kwa hamasa kiliunga, mijini wakaamka,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Kabla hajafariki, watesi waliinuka,
Na hao wakahakiki, Biko asijesikika,
Mjini kwake abaki, asije akaondoka,
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Lile la kujiuliza, lenye majibu hakika,
Kile Biko aliwaza, ili kiweze kufika,
Tunaweza kutangaza, huku tunachangamka?
Mpigania uhuru, anakumbukwa daima.
Steve Biko - Anakumbukwa daima
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment