KINA MANDELA NI WENGI - 4
Moja tisa tisini, karudi kwao nyumbani,
Silaha kuwekwa chini, kwa mjadala mezani,
Mandela wa Gerezani, kawa huru mtaani,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Huku tunasubiria, ya kwamba tuwe shangweni,
Habari tunakasikia, Hani kaenda kifoni,
Watu limmiminia, risasi nyingi mwilini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Kufwatia kifo chake, huyu bingwa Chris Hani
Ona taharuki yake, nchi kuwa matatani,
Sababu ya kazi yake, ukombozi wa kusini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Mtiti ungetokea, nchi kuwa hatarini,
Lakini ulipotea, kwa Mandela hadharani,
Vile alielezea, ubaya wao wahuni,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Wauaji ni wawili, waliomuua Hani,
Wamelileta timbwili, nchini na duniani,
Tupokee hii hali, tupalilie amani,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Alivyowaomba watu, kama yu madarakani,
Walisikiliza watu, utulivu mitaani,
Walakini hiki kitu, liumiza mioyoni,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Wale wazungu wawili, waliomuua Hani,
Hukumu yao kamili, lipotiwa hatiani,
Kifo kiliwakabili, kulipa wao uhuni,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Tume ya Maridhiano, ya Afrika Kusini,
Sheria kutiwa wino, adhabu kifo kapuni,
Wakapatiwa kibano, cha maisha gerezani,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Watu hawakutulia, mijadala ya mezani,
Mwaka ulipofikia, demokrasia nchini,
Hani ndiyo alifia, akienda kaburini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Sasa ni huru Afrika, ukoloni uko chini,
Mengine twataabika, ya haki pia amani,
Sababu kwenda vitani, zingine bado hewani,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Wakati anauawa, Komrade Chris Hani,
Kwa kweli alijaliwa, maarufu kileleni,
Wa pili kuangaliwa, huko Afrika Kusini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Chris HaniMtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment